0

Simba yatambia usajili wake

Simba yatambia usajili wake

Wed, 2 Sep 2020 Source: HabariLeo

MJUMBE wa Bodi ya wakurugenzi wa Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kwa usajili walioufanya safari hii wanaamini wanaenda kupeperusha bendera ya nchi vyema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alisema kwa sasa uongozi wa Simba unasimamia kuhakikisha wachezaji wanaandaliwa kwa uaminifu na kwa weledi wa kutoa ushindani kwa timu zingine.

Akizungumza jana Try Again alisema malengo yao ni kutinga kwenye hatua ya makundi kwenye michuano hiyo na baada ya hapo wataangalia.

“Dalili ya mvua ni mawingu tumeanza vyema kwa kuchukua Ngao ya Jamii na kwa usajili tuliofanya tunaamini tutapeperusha bendera ya nchi vyema, kwenye ligi ya mabingwa Afrika, kikubwa tunawaanda wachezaji ili tufikie hatua ya makundi ndiyo malengo yetu”alisema Try Again.

Alisema mbali na kudhamiria kufanya makubwa kimataifa lakini bado wanatamani kufanya makubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ili kutetea ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.

Try Again amewaomba mashabiki wa mabingwa hao kuwa watulivu kwenye kipindi hiki ambacho benchi la ufundi linafanya kazi yake ya maandalizi kwa wachezaji wapya na wazamani.

Simba imepata tiketi ya kuiwakilisha nchi baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Chanzo: HabariLeo