0

Simba mjengoni kuteta na Mo

02e6b39e98963372679f0589c3a82155 Simba mjengoni kuteta na Mo

Wed, 18 Nov 2020 Source: HabariLeo

WANACHAMA wa Simba tawi la Bunge ‘Simba mjengoni’ wanatarajiwa kukutana na Mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji na Mkurugenzi, Barbara Gongalez kujua maendeleo ya klabu.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa tawi la Simba mjengoni, ambaye pia ni Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi na kusema leo wanatarajia kukutana kwa hafla ya chakula cha usiku ambapo atakuwepo, Mohamed Dewji na Barbara Gongalez ambao watatoa maendeleo ya klabu na mikakati ya Simba kufikia.

Mbali na hilo pia Shangazi alisema watatumia hafla hiyo kusajili wanachama wapya wa Bunge la 12.

Alisema hafla hiyo inayojulikana kwa jina la Simba Mjengoni get-together itaongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai huku wageni wengine wanaotarajia kuwepo ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

" Kama mnavyojua hapa bungeni tuna tawi kwa wabunge wapenzi wa Simba, na kwa sasa tumeanza Bunge la 12 na kuna wabunge wapya hivyo tutatumia hafla ya chakula cha usiku kusajili wanachama wapya,”.

" Lakini pia katika hafla hiyo atakuwepo Mwekezaji wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji na Mkurugenzi Barbara Gongalez ambao watatupa maendeleo ya klabu na mikakati ya kuifanya Simba kufikia kiwango kingine."

Naye meneja wa benki ya Equity mkoa wa Dodoma, Upendo Makula alisema benki yake kwa kushirikina na Simba wamekuwa wakitoa kadi za uanachama na mpaka sasa wanachama 1,000 wamesajiliwa.

Alisema kupata kadi ya Simba kupitia benki ya Equity, mwanaSimba anapaswa kulipia Sh 22,000 ambapo Sh 10,000 ni gharama za kadi na Sh 12,000 zinakwenda moja kwa moja kwenye klabu ikiwa ni mchango wake kwa mwaka mmoja.

Makula alisema kwa mwanachama ambaye hana kiasi hicho, anapaswa kutoa kwanza Sh 5,000 na baadaye kutoa kidogo kidogo na kumaliza kiasi hicho ndani ya mwezi na atapewa kadi yake ya uanachama.

"Kuna faida kwa mwanachama anayepata kadi hizi, kwanza atakuwa na fursa ya kupata punguzo anapofanya manunuzi kwenye maduka makubwa lakini inakuwa ni nafasi ya mwanachama kuchangia klabu yake "

"Shabiki na mwanachama mzuri ni vizuri kuwa na kadi na huo ndio uzalendo kwa timu yako, hivyo kadi hizi zinapatikana kwenye matawi ya Equity na sehemu ambako hakuna tawi, basi benki unaweza kufanya utaratibu wa kuipata."

Klabu ya Simba imevuna Sh milioni 12 kutoka kwa wanachama 1,000 walionunua kadi za uanachama kupitia kupitia Benki ya Equity mkoa wa Dodoma pekee.

Chanzo: HabariLeo