0

Simba, Namungo zapangua ratiba Ligi Kuu

Simba, Namungo zapangua ratiba Ligi Kuu

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

BODI ya Ligi Tanzania (TPLB) imefanya mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuziwezesha Simba na Namungo FC kushiriki vizuri mashindano ya kimataifa.

Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika imepangwa kucheza dhidi ya Plateau United ya Nigeria katika mchezo utakaofanyika baadae mwezi huu.

Namungo FC wenyewe watacheza dhidi ya timu ya Sudan Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kutokana na mabadiliko hayo ya ratiba, mchezo kati ya Dodoma Jiji dhidi ya Simba uliokuwa upigwe Novemba 24 umesogewa mbele ili kuwapa nafasi Wekundu hao wa Msimbazi kujiandaa na mchezo wa hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya wababe hao wa Nigeria.

Jumamosi Novemba 21 Simba itacheza na Coastal Union mkoani Arusha kabla ya safari ya kuelekea nchini Nigeria kuikabili Plateau United kwenye mchezo ambao utapigwa mwishoni mwa mwezi huu.

Namungo wao walipaswa kucheza na KMC Novemba 24 lakini mchezo wao umesogezwa mbele ili wapate nafasi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya wapinzani wao wa michuano ya Kombe la Shirikisho kutoka Sudan Kusini.

Bodi ya Ligi awali ilitangaza kuwa haitabadili ratiba ya ligi kwa kile ilichosema wamezingatia mechi za kimataifa kwa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa kwa klabu na timu za taifa kitu ambacho ni tofauti kwa sasa.

Chanzo: HabariLeo