0

Shime: Taji limetupa deni kwa Watanzania

Shime: Taji limetupa deni kwa Watanzania

Tue, 17 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By Charles AbelDar es Salaam. Wakati benchi la ufundi la timu za wanawake likiweka rekodi ya kutwaa taji la tano baada ya ile ya miaka 17 kutwaa taji la Cosafa, kocha Bakari Shime amedai kuwa taji hilo limewapa deni kubwa kwa Watanzania.

Akizungumza jana baada ya kuwasili jijini Dar es Salaa wakitokea Afrika Kusini ilikotwaa taji hilo, Shime alisema kuwa hawawezi kubweteka na mafanikio waliyoyapata na badala yake wana kazi kubwa mbele yao.

“Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kupata taji hili na mengine hapo nyuma, lakini hili kwetu tunaamini limetufanya tuwe na deni kubwa ambalo tunapaswa kuhakikisha tunalilipa kwa Watanzania.

“Deni lenyewe ni kuhakikisha timu zetu za wanawake zinafuzu na kushiriki fainali za Afrika, lakini pia zile za Kombe la Dunia, jambo ambalo si jepesi lakini tunatakiwa kulifanya,” alisema Shime.

Hilo ni taji la tano kwa benchi la ufundi la timu za taifa za wanawake nchini linaloongozwa na Shime na msaidizi wake, Edna Lema, kwani kabla ya hapo waliziongoza kutwaa mataji manne tofauti.

Mataji hayo ni Kombe la Cecafa kwa wanawake 2016 na 2018, Kombe la Michezo ya Afrika Mashariki 2018 na Kombe la Cosafa kwa wanawake chini ya umri wa miaka 20.

Chanzo: Mwanaspoti