0

Serengeti Boys mzigoni Morocco leo

Serengeti Boys mzigoni Morocco leo

Sat, 14 Nov 2020 Source: HabariLeo

KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kinatarajia kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji Morocco leo asubuhi.

Mchezo huo ni wa kwanza tangu kikosi hicho kiwasili mjini Rabat, kuweka kambi ya kujiandaa na michuano ya kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, Cecafa, kwa vijana wa umri huo.

Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Kigali, Rwanda kuanzia Desemba 13- 28.

Akizungumza kutoka Morocco kwa njia ya mtandao kocha wa kikosi hicho Hababuu Ali alisema huo ni mchezo wao wa kwanza wa kimataifa na wamejipanga kuutumia vizuri kuona makosa na kuyasahihisha.

“Tunacheza na Morocco, hii ni mechi yetu ya kwanza ya kimataifa sasa tutaitumia vizuri ipasavyo kuona makosa na kuyasahihisha, lengo ni kujipima na kuona nini tunacho na nini hatuna,”alisema Ali.

Alisema tangu wamewasili nchini humo wanafanya mazoezi asubuhi na jioni na kikosi kina morali kubwa kuelekea kwenye mchezo huo ambao wanaamini utakuwa kipimo sahihi kwa wachezaji wake.

Alisema mchezo huo unatarajiwa kuchezwa leo, saa saba mchana.

“Kwa mujibu wa ratiba tulivyopangiwa ni mechi mbili tunatakiwa kucheza kesho (leo) na tutarejeana wiki ijyao,” alisema.

Alisema hali ya hewa ni rafiki kwa wachezaji wake siyo ya joto wala baridi kali ila ipo katikati na ni moja ya sababu inayowapa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mechi dhidi ya wenyeji wao.

Chanzo: HabariLeo