0

Sare yamuibua kocha Yanga

Sare yamuibua kocha Yanga

Tue, 8 Sep 2020 Source: HabariLeo

KOCHA mpya wa Yanga, Zlatko Karmpotic, amekiri kuanza vibaya Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, katika mchezo uliofanyika juzi Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumzia mchezo huo, kocha huyo raia wa Serbia alisema wachezaji wake kutokaa pamoja kwa muda mrefu, pamoja na kutokuwa na muda wa kutosha wa maandalizi kabla ya kuanza kwa ligi, ni sababu ya timu yake kuanza kwa sare.

Alisema huo sio mwanzo mzuri kwa timu yoyote yenye lengo la kuwania ubingwa.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Karmpotic alisema wachezaji kutokukaa pamoja kwa muda mrefu kulisababisha wachezaji wake kukosa muunganiko kuelekea kwenye lango la wapinzani wao.

“Kutoka sare sio matokeo mazuri, lakini sababu iliyochangia matokeo haya ni wachezaji wangu hawajakaa pamoja kwa muda mrefu na kutengeneza muunganiko ambao umeonekana kukosekana kwenye mechi yetu ya leo (juzi) dhidi ya wapinzani wetu. Wachezaji wengi walijiunga na kikosi siku moja kabla ya ligi kuanza,” alisema Karmpotic.

Alisema wachezaji wake wengi hawakuwa na uwezo wa kupambana muda wote wa dakika 90 hususani wazawa ambao walikosa utimamu wa mwili ili kukabiliana na wapinzani wao ambao walikuwa bora katika kila idara.

Pia Karmpotic alisema kuchelewa kupata vibali kwa baadhi ya wachezaji wa kimataifa ni sababu iliyomfanya kuwapa nafasi ya kuanza kucheza wachezaji wazawa.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali kutoka pande zote mbili, ilishuhudiwa Yanga wakisawazisha dakika ya 20 kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Michael Surpong, baada ya Prisons kutangulia kupata bao dakika ya saba lililofungwa na Lampart Sabiyanka.

Baada ya mchezo huo kikosi cha Yanga kinajipanga kwa mchezo unaokuja wa muendelezo wa ligi hiyo dhidi ya Mbeya City utakaopigwa kwenye uwanja huo huo.

Chanzo: HabariLeo