0

Samatta aja kivingine

Samatta aja kivingine

Thu, 10 Sep 2020 Source: HabariLeo

MCHEZAJI wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na klabu ya Aston Villa ya England, Mbwana Samatta, kwa ushirikiano na kampuni ya Korea ya Paymaker, amezindua kiteknolojia ya kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao iitwayo Samapay.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, Samatta alisema lengo la Samapay ni kuwawezesha wananchi kunufaika na kila malipo wanayofanya kutoka kwa wauzaji wanatumia mfumo wa Samapay Merchant.

Alisema mtumiaji anaweza kufanya manunuzi katika migahawa, maduka au kupata huduma katika saluni, ambapo ili kupata huduma hiyo iatatakiwa kupakua ‘Apps’ ya duka mtandaoni ya Samapay inayopatikana Google Play Store.

“Mteja mwenye Samapaya anapata punguzo la asilimia kulingana na makubaliano na muuzaji husika, ambapo wapo wauzaji ambao wanatoa punguzo la asilimia tano, wengine 10 na kuendelea, hivyo muuzaji mwenye Samapay Merchant atamwekea mteja asilimia husika kama pointi katika akaunti yake ya Samapay, hayo yatafanyika kwa kunakili ‘QR’ ya mteja moja kwa moja,” alisema.

Samatta alisema pointi tano zinazoingizwa kwenye Samapay ya mteja kutoka kwa muuzaji zitamwezesha kupata huduma nyingine ambayo thamani yake inalingana na wingi wa pointi atakazokuwa amekusanya.

“Mfano bidhaa inauzwa Sh 10,000, mteja anayetumia Samapay akifanya malipo kwa kutumia mfumo huu atapata punguzo la asilimia tano, hivyo atalazimika kulipa Sh 9,500 na Sh 500 inayobakia ambayo inakuwa pointi yenyewe anawekewa mteja,” alisema Samatta.

Alisema mteja akikusanya pointi nyingi zaidi anaweza kuzitumia kuchukulia bidhaa nyingine zenye thamani sawa na wingi wa pointi atakazokuwa nazo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mikakati wa Samapay ambaye ni Mkuu wa Utawala wa Mradi wa Samagoal wa mchezaji huyo, Emmanuel Massawe, alisema Samapay ni kitu kikubwa ambacho timu nzima ya wafanyakazi wa mchezaji huyo imefurahi kujiunga nayo.

Alisema ni furaha kuwa sehemu ya mradi huo kwa kuwa umekuja kuleta mabadiliko nchini na kwamba baadaye mteja ataweza kufanya malipo moja kwa moja kutoka katika Samapay.

Alisema maeneo ambayo mteja anaweza kuhudumiwa kwa kutumia Samapay ni Regency Park Hotel, Menbase, The rub spa, Terrace Lounge & Restaurant, Atsoko, Scott’s pizza na Mimi beauty salon, zote za Dar es Salaam

Chanzo: HabariLeo