0

Ruvu, Kagera, Gwambina zatakata Ligi Kuu

Ruvu, Kagera, Gwambina zatakata Ligi Kuu

Thu, 26 Nov 2020 Source: HabariLeo

RUVU Shooting, Kagera Sugar na Gwambina zimeibuka na pointi tatu muhimu baada ya kushinda mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye viwanja tofauti jana.

Ruvu Shooting wameshinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons wakati Kagera Sugar wameshinda 3-0 dhidi ya Biashara United ya Musoma mkoani Mara na Gwambina FC ikiwa ugenini imeshinda 4-3 dhidi ya Mwadui FC.

Bao pekee la Ruvu Shooting lilifungwa na Mussa Abdulrahman katika dakika ya 30 na kuiwezesha timu hiyo kufikisha pointi 22 na kuwa katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 18.

Katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, wenyeji Kagera Sugar walitumia vizuri uwanja wao wa nyumbani baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi Biashara na kuifanya timu hiyo kufikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi 12.

Mabo ya Kagera Sugar yalifungwa na Erick Mwaijage katika dakika ya 10 wakati la pili likiwekwa kimiani na Nassoro Kapama katika dakika ya 77 na lile la ushindi likifungwa na Hassan Mwaterema katika dakika ya 78.

Kwa upande wa Gwambina waliokuwa ugenini, mabao hayo yalifungwa na Jimson Stephen katika dakika ya sita, Jacob Massawe katika dakika ya 26 na 66 na Ibrahim Meshack katika dakika ya 45 yale ya Mwadui yalifungwa na Herman Masenga dakika ya 15, Salum Chabi dakika ya 39 na Ismail Ally dakika ya 62.

Ligi hiyo itaendelea tena Jumamosi kwa Dodoma Jiji kuikaribisha Ihefu katika mchezo wa Ligi Kuu utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, huku Mbeya City wakiwa na kibarua cha kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar na Yanga watakwaana na JKT Tanzania.

Chanzo: HabariLeo