0

Rocky City Marathon yapata mdhamini

Rocky City Marathon yapata mdhamini

Wed, 11 Nov 2020 Source: HabariLeo

KAMPUNI ya Magare inayohusika na uhandisi wa umeme na mitambo ya viwandani pamoja na migodini imedhamini mashindano ya mbio za Rock city marathon kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 15/- katika kufanikisha mbio hizo zitakazofanyika Novemba 29 mwaka huu, viwanja vya Rock city mall.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mabula Magangila ameseman udhamini huo unalenga kuunga mkono jitihada za wadau wengine pamoja na Serikali kwa ujumla katika kuhamasisha michezo ya ndani pamoja na utalii.

Amesema kampuni yake itaendelea kushirikiana na waandaaji wa mbio za hizo kuhakikisha zinafanikiwa kuvutia zaidi washiriki kutoka nje na ndani ya nchi ambao ujio wao jijini Mwanza utasaidia kukuza utalii.

Kwa upande wake, Mratibu wa mbio za Rock city marathon, bMagdalena Laizer ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo.

Amesema wanatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 3000 wakiwemo wakimbiaji wa kimataifa,wanafunzi na watu wenye ualibino ambao watakimbia kilimita 5.

Ameongeza kuwa usajili bado unaendelea kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yao na vituo vya kawaida katika mikoa ya Mwanza,Geita,Simiyu,Shinyanga,Dodoma,Arusha na Dar-es-salaam.

Washindi wa kwanza wa kilomita 21 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia shilingi milioni 2, mshindi wa pili atachukua milioni 1.3/- na tatu atachukua 700,000/-.

Amesema kuwa washindi wa kilomita 10 hawatakuwa na zawadi za fedha taslimu isipokuwa washiriki watajipati fulana na medali.

Chanzo: HabariLeo