0

Pamba mechi tisa tu freshi

Thu, 10 Sep 2020 Source: mwanaspoti.co.tz

By SADDAM SADICKMWANZA. KOCHA Mkuu wa Pamba, Ulimboka Mwakingwe amesema licha ya mechi tatu walizocheza kujipima nguvu, lakini bado hajaridhika na kiwango cha nyota wake, hivyo anahitaji michezo nyingine tisa ili kujiweka sawa na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) itakayoanza Oktoba 3.

Katika mechi hizo tatu mabingwa hao wa zamani wa Tanzania, kabla ya kushuka daraja mwaka 2000 imetoka sare ya 2-2 dhidi ya Mwanza Combine, kisha kuzifunga Copco Veteran FC mabao 5 -0 na Nyamagana United kwa 4-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwakingwe alisema pamoja na matokeo mazuri waliyopata katika mechi hizo za kirafiki, lakini bado hajafurahia muunganiko wa timu yake, hivyo anaendelea kusaka michezo mingine.

Alisema mipango yake kwa sasa ni kucheza mechi nyingine tisa zikiwamo timu za Ligi Kuu ili kumuwezesha kubaini mapungufu ya kiufundi ili Ligi itakapoanza wafanye kweli.

“Bado sijaridhika na ubora wao haswa muunganiko, ukiangalia kikosi chote sura ni mpya kwahiyo nahitaji michezo kama tisa nyingine za kirafiki ili kujihakikishia kuwa sawa na Ligi,” alisema Kocha huyo.

Mwakingwe aliongeza kinachompa nguvu ni kutokana na usajili alioufanya kwa kushirikia na uongozi, hivyo anaamini Ligi itakapoanza huenda Pamba ikaandika histroria nyingine ya kuungana na Simba na Yanga.

Chanzo: mwanaspoti.co.tz