0

Osaka ajitoa French Open

Osaka ajitoa French Open

Sat, 19 Sep 2020 Source: HabariLeo

BINGWA wa US Open, Naomi Osaka amejitoa kwenye michuano ya French Open inayotarajiwa kuanza Septemba 27 mwaka huu.

Jumamosi iliyopita, Mjapani huyo alishinda taji la pili la US Open na la tatu la Grand Slam kwa ushindi wa 1-6 6-3 6-3 dhidi ya Victoria Azarenka mjini New York.

Alisema kwenye taarifa yake: “Sitakuwa tayari kucheza French Open.” “Bado nasumbuliwa na tatizo la misuli kwa hiyo sina muda wa kutosha kujiandaa, michuano hii miwili imekuja karibu karibu mno.

” Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alikutwa na tatizo la misuli ya kushoto katika mechi ya fainali ya US Open alipomfunga Azarenka Flushing Meadows.

Mchezaji huyo namba tatu duniani, ambaye alishinda taji la Australian Open mwaka 2019 hajawahi kusonga mbele kwa zaidi ya raundi tatu kwenye viwanja vya Roland Garros.

Mapema mwezi huu, mchezaji namba moja duniani Ashleigh Barty alitangaza kutotetea taji la French Open akijitoa kwenye michuano kutokana na janga la virusi vya corona.

Kwa upande wa wanaume, mshindi mara wa 20 wa Grand Slam, Roger Federer ndiye mchezaji mkubwa zaidi atakayekosekana akijiuguza goti lake lililofanyiwa upasuaji.

Juzi, waandaaji wa French Open walipunguza idadi ya mashabiki wanaoruhusiwa kuangalia mechi kufikia 5,000 kutokana na kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona.

Michuano hiyo ya Paris ilisogezwa mbele, awali ilipangwa kufanyika Mei 24 lakini kutokana na janga la corona ikasogezwa mpaka mwisho wa mwezi huu.

Chanzo: HabariLeo