0

Ni Mwakinyo na Paz leo

Ni Mwakinyo na Paz leo

Fri, 13 Nov 2020 Source: HabariLeo

BONDIA Hassan Mwakinyo leo anatarajiwa kuipeperusha bendera ya Tanzania katika pambano la kuwania mkanda wa Chama cha Kimataifa cha Ndondi (WBF) dhidi ya Muargentina, Jose Paz.

Pambano hilo la mzunguko wa 12 uzito wa super welter ubingwa wa mabara litachezwa katika ukumbi wa Next Door Arena, Dar es Salaam.

Mwakinyo ndiye bingwa mtetezi wa mkanda huo hivyo anahitaji kuutetea ili kuendelea kuwa katika ubora utakaomuongezea thamani.

Akizungumzia maandalizi yake bondia huyo alisema amejiandaa vizuri kwa mazoezi ya kutosha kumpiga mpinzani wake.

“Nimejipanga vizuri kikubwa mashabiki wangu wajitokeze kwa wingi nawaahidi sitawaangusha,” alisema.

Mwakinyo ameshinda mapambano karibu yote yaliyoandaliwa katika ardhi ya nyumbani ingawa pia mpizani wake sio mbaya.

Rekodi ya Paz inaonesha amecheza mapambano 35 na kati ya hayo, ameshinda 23, amepoteza 11 na kupata sare moja.

Bondia huyo amepoteza mapambano karibu manne ya karibuni aliyocheza ugenini ambayo yanaweza kushusha zaidi kiwango chake.

Mabondia wengine watakaochuana kusindikiza pambano hilo ni Hussein Itaba dhidi ya Alex Kabangu wa DR. Congo, Fatuma Zarika dhidi ya Patience Mastara (Zimbabwe) na Mtanzania Zulfa Macho ambaye atazichapa na Alice Mbewe wa Zambia.

Chanzo: HabariLeo