0

Ngorongoro Heroes kujipima na Sudan

Ngorongoro Heroes kujipima na Sudan

Sun, 8 Nov 2020 Source: HabariLeo

TIMU ya Soka ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, leo inatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Timu hizo zinatumia mechi hiyo kujiandaa na michuano ya Afrika Mashariki na Kati inayotarajia kufanyika kuanzia Novemba 20-Desemba 10, mwaka huu jijini, Arusha.

Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Jamhuri Kihwelo 'Julio' aliliambia gazeti hili jana kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na anaamini watafanya vyema dhidi ya wageni wao Sudan.

Julio alisema amewaandaa wachezaji wake kucheza soka la utulivu na kutumia dakika za mapema kuwasoma wapinzani wao na baadaye wataongeza kasi kulingana na mfumo watakaoutumia.

Alisema anatarajia kutoa nafasi kwa wachezaji wake katika mechi hiyo ili kufahamu walivyoyapokea mafunzo yake.

Sudan iliwasili nchini tangu juzi, ikitokea Nairobi Kenya walipoweka kambi ya muda mfupi.

Baada ya mechi dhidi ya Sudan, Ngorongoro Heroes inatarajiwa kwenda Zanzibar kucheza michezo mingine ya kujipima nguvu.

Chanzo: HabariLeo