0

Ngassa, Tegete waachiwa msala

Thu, 3 Sep 2020 Source: mwanaspoti.co.tz

MABOSI wa Ndanda wameanza maandalizi yao ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kushuka kutoka Ligi Kuu msimu uliopita na fasta wakapata wazo la kuwavuta majembe ya maana hususani wakongwe kina Henry Joseph Shindika, Mrisho Ngassa na Jerry Tegete ili kuwapa kazi ya kupandisha daraja.

Nyota hao wa zamani wa kimataifa waliowahi kukipiga Simba na Yanga, wameachiwa msala wa kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu wakiwa miongoni mwa orodha ya majina ya waliosajiliwa msimu huu.

Mbali na Ngassa aliyetemwa na Yanga, Joseph kutoka Mtibwa Sugar na Tegete aliyekuwa Alliance, Ndanda pia imenasa saini za wazoefu, William Lucian ‘Gallas’ (Polisi Tanzania), Stamili Mbonde (Mtibwa Sugar) na Paul Ngalema (Lipuli) wote kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Ngassa, Gallas na Ngalema walishawahi kuichezea timu hiyo kwa vipindi tofauti siku za nyuma na ni wachezaji waliokuwa wakipata nafasi katika timu zao zilizowaacha sambamba na Henry Joseph.

Katibu wa timu hiyo, Seleman Kachele alisema lengo la kuwasajili wachezaji hao ni kuhakikisha kwamba msimu ujao wanarejea katika Ligi Kuu.

“Ni kweli tumewasajili mkataba wa mwaka moja kila moja, hawa ni wachezaji wazoefu tukiwachanganya na wale vijana basi tuna imani kabisa msimu ujao tunarudi Ligi Kuu,” alisema katibu katika mikakati yao.

Chanzo: mwanaspoti.co.tz