0

Ndayiragije atoa masharti kufuzu Afcon

Ndayiragije atoa masharti kufuzu Afcon

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Etienne Ndayiragije amesema bado ana imani wanaweza kufanya vizuri na kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) kama tu baadhi ya mambo yatazingatiwa na kupewa kipaumbele.

Ndayiragije aliyasema hayo juzi baada ya timu yake kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Alitaja mambo muhimu ili waweze kufuzu ni kuhakikisha wanapata maandalizi mazuri na nguvu ziwekezwe kwenye timu ya taifa, huku akitolea mfano kama ambavyo klabu kubwa zinavyofanyiwa.

“Ikiwa tutahitaji kwenda mbele zaidi tuongeze maandalizi na ufanisi ambao tunafanya kupata matokeo tofauti na yaliyopita,” alisema na kuongeza: “Tukiendelea kujiandaa na kuwekeza nguvu kwa timu yetu ya taifa natolea mfano jinsi tunavyoandaa klabu nina imani vipaji vipo tutafanya vizuri,” alisema.

Jambo jingine muhimu alisema kuna haja ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi kufuatiliwa ikiwezekana waitwe wote ili kutengeneza timu nzuri yenye ushindani.

“Tuwezeshwe na kufika mbali halafu wengine wakiwa wanacheza huko nje tuwaangalie ili kupata timu nzuri,” alisema.

Katika Kundi J, kinara ni Tunisia yenye pointi 10 na tayari imefuzu, ikifuatiwa na Guinea ya Ikweta pointi sita, Tanzania pointi nne na Libya pointi tatu na kila mmoja imeshacheza michezo minne na na kubakisha miwili na zote zina nafasi ya kufuzu.

Tanzania katika mchezo ujao inatacheza na Guinea ya Ikweta ugenini, mchezo utakaochezwa Machi mwakani kisha baadaye itamaliza na Libya nyumbani.

Kocha Ndayiragije alisema kabla ya kukutana na Guinea kutakuwa na michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani Chan 2021 na kuomba maandalizi yafanyike mapema tna waitwe wachezaji wa ndani na wa nje ili kuandaa muunganiko mzuri.

Kuhusu mchezo uliopita dhidi ya Tunisia, aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonesha jitihada kwani hawakuwa na muda mzuri wa maandalizi.

“Nawapongeza wachezaji wangu wamejaribu kutoa kile walichokuwa nacho kwa kweli nikiangalia kile tulichowekeza na kulinganisha na kile ambacho wametoa wanastahili pongezi, niliwahimiza kujiamini na kufuata tuliyofanyia kazi kwenye mazoezi na jinsi muda ulivyokuwa unaenda wakawa wanabadilika,” alisema.

Pia alimzungumzia mshambuliaji Adam Adam aliyecheza kwa mara ya kwanza kwenye timu ya taifa, akisema kuna kitu ameonesha, ni mtu anayejitaji maandalizi zaidi na akiweza kuonesha zaidi ni mchezaji mzuri.

Chanzo: HabariLeo