0

Mwanza yapania kikapu Taifa Cup

Mwanza yapania kikapu Taifa Cup

Thu, 12 Nov 2020 Source: HabariLeo

CHAMA cha Mpira wa Kikapu Mkoani Mwanza (MRBA) kimesema timu zake zote mbili za wanaume (Rockity Heroes) na ya wanawake (Mwanza ladies) zimejipanga kutwaa ubingwa wa mashindano ya Taifa ya mpira wa kikapu yanayotarajia kuanzia leo katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Mratibu wa mashindano wa MRBA, Haidari Abdul jana alisema timu zao zote mbili zimejipanga kutwaa ubingwa huo.

Alisema timu ya wanaume itawakilishwa na wachezaji 12 na itakuwa chini ya Kocha Mkuu, Benson Nyasebwa na ya wanawake itakuwa chini ya Kocha Paschal Nkuba.

Alisema anawaomba wapenzi wa mchezo wa mpira wa kikapu kutoka mkoa wa Mwanza wajitokeze kwa wingi jijini Dodoma kuzishangilia timu zao ili ziweze kufanya vyema katika mashindano hayo.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Bugando Profile na Mwanza Dolphins alisema baada ya mashindano ya Kombe la Taifa, chama hicho kitaendelea na mashindano ya Ligi ya Mkoa.

Mashindano hayo yatahusisha timu 24 za wanaume na timu ya jiji la Mwanza (Rock City Heroes) imepangwa pamoja na timu za Mbeya, Kigoma, Manyara, Pwani na Kinondoni.

Chanzo: HabariLeo