0

Mwakinyo sasa ni ubingwa wa dunia

Mwakinyo sasa ni ubingwa wa dunia

Mon, 16 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

Mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini Ijumaa Novemba 13,2020 walishuhudia mapinduzi makubwa katika mchezo wa ngumi za kulipwa kwa kufanyika pambano la kwanza la limataifa kwenye ukumbi wa kisasa wa Next Door Arena, Oysterbay.

Katika pambano hilo lililoandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports , bondia Hassan Mwakinyo alitetea vyema ubingwa wake mabara wa uzito wa Super Welter wa WBF baada ya kumchapa kwa TKO mpinzani wake Jose Carlos Paz wa Argentina katika raundi ya nne.

Ni mapinduzi kutokana na ukweli kuwa mapambano ya ngumi za kulipwa nchini kwa miaka mingi huwa yanafanyikia kwenye kumbi za ‘kawaida sana’ tofauti na wenye hadhi ya kimataifa kama wa Next Door Arena.

Ni mapinduzi vile vile kutokana na waandaaji kufanikiwa kuongeza wigo wa wadau wa mchezo wa ngumi za kulipwa nchini tokea kwenye asili yake kama vile Keko, Manzese (Friends Corner), Mabibo, Kinondoni Mkwajuni, Mwananyamala na eneo la Kwa Msisiri.

Miaka ya nyuma, mapambano makubwa ya ngumi za kulipwa yalikuwa yanafanyikia kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee , lakini kwa siku za hivi karibuni, uwanja wa Uhuru, PTA na mara moja tu kwenye Mlimani City.

Kumbi za zamani kama Kolini (Tandale), Friends Corner Hotel, Vijana Social, DDC Mlimani, King Palace (Keko), Texas (Manzese), Relwe Gerezani na nyinginezo zilikuwa maarufu sana kwa mapambano ya ngumi za kulipwa.

Chanzo: Mwanaspoti