0

Mwakinyo apewa ulaji

Mwakinyo apewa ulaji

Thu, 12 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By Imani MakongoroDar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa la Dunia (WBF), Goldberg Howard amesema kama bondia Hassan Mwakinyo atatetea ubingwa wa Shirikisho hilo wa mabara kesho, atakidhi viwango vya kuwania ubingwa wa dunia.

Howard ametamka hayo jana alipowasili nchini sanjari na mwamuzi wa kimataifa, Edward Marshal kutoka Afrika Kusini ili kusimamia pambano la Mwakinyo na Jose Carlos Paz wa Argentina litakalopigwa kwenye Ukumbi wa Next Door Arena, Dar es Salaam.

Mwakinyo atapanda ulingoni kutetea ubingwa wa mabara wa WBF kwenye uzani wa super welter, pambano la raundi 10 likalochezeshwa na Marshal na kusimamiwa na Howard sanjari na viongozi wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC).

Akizungumza baada ya kuwasili nchini akiwa na mkanda ambao Mwakinyo na Paz watagombea, Howard alisema kama Mtanzania huyo atashinda, itakuwa ni fursa kwake kuwania mkanda wa dunia Februari mwakani.

“Atacheza na bondia kutoka Georgia, Lasha Gurguliani, lakini kama atautetea ubingwa wake wa mabara kesho, kinyume na hapo hawezi kupata nafasi hiyo,” alisisitiza Howard, ambaye amewasili nchini na vifaa ikiwamo glovu mpya ambazo ndizo Paz na Mwakinyo watavitumia ulingoni.

Howard pia amewapongeza waandaaji, kampuni ya Jackson Group Sports kwa kutimiza sheria na kanuni zote za WBF kuandaa pambano hilo la ubingwa linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa ndondi nchini.

Chanzo: Mwanaspoti