0

Murray arejea kwa kishindo US Open

Thu, 3 Sep 2020 Source: habarileo.co.tz

ANDY Murray amerejea kwa kishindo katika kiwango chake cha ubora baada ya kushinda mchezo wake dhidi ya Yoshihito Nishioka wa mashindano ya US Open katika raundi ya kwanza, baada ya kusubiri kwa muda mrefu kurejea kwa mashindao makubwa ya tenisi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, awali mshindi huyo alikuwa nyuma kwa seti mbili na baadaye kumchakaza Mjapani huyo na kushinda kwa 4-6 4-6 7-6 (7-5) 7-6 (7-4) 6-4.

Muingereza Murray, ambaye mchezo wake wa mwisho wa mchezaji mmoja mmoja ulikuwa mwaka 2019 wa mashindano ya Australian Open kabla ya kukaa pembeni kufuatia upasuaji, aliuanza vibaya mchezo huo.

Lakini alipambana na kujikuta akiibuka na ushindi mnono katika mchezo huo wa aina yake.

Mskotishi huyo awali alipata ushindi kwa muda wa saa nne na dakika 39, sasa atakabiliana na Mcanada anayeshikilia nafasi ya 15 katika ubora, Felix Auger-Aliassime, katika mchezo wa raundi ya nne.

Akicheza katika uwanja mtupu na uliotulia wa Arthur Ashe, Murray alishinda mchezo huo, baada ya kushinda taji kubwa la mwisho 2012.

Mtangazaji wa Radio ya BBC, David Law alisema: "Andy Murray haonekani kabisa kama Andy Murray," akimaanisha hakuonesha makeke yake kama aliyokuwa akifanya huko nyuma.

Murray amekuwa Muingereza wa pili baada ya muda mrefu kutetea pointi zake licha ya kuwa nyuma kwa seti mbili, baada ya Cameron Norrie kufanya kama hivyo alipocheza dhidi ya Diego Schwartzman.

Katika mchezo wake wa mwisho wa mashindano makubwa kwa mchezaji mmoja mmoja Januari, 2019, Murray alijikuta akibubujikwa na machozi wakati akisema anahofia kustaafu kucheza kwa sababu ya maumivu makali ya nyonga.

Lakini baadae mwezi huohuo alifanyiwa upasuaji na baada ya kukaa nje kwa miezi mitano alirejea uwanjani, akicheza mashindano ya wachezaji wawili wawili ya taji la Queen akiwa na Feliciano Lopez.

Alicheza dablo na dablo mchanganyiko katika mashindano ya Wimbledon mwaka huo na baadae alirudi katika mashindano Agosti 2019.

Chanzo: habarileo.co.tz