0

Mugalu arejea kikosini Simba

Mugalu arejea kikosini Simba

Wed, 4 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By THOBIAS SEBASTIANSTRAIKA wa Simba, Chris Mugalu amepangwa kikosi cha timu hiyo kitakachocheza na Kagera Sugar ingawa awali ilidaiwa kwamba mchezaji huyo hayuko fiti kwani alikuwa anasumbuliwa na majeraha.

Kocha wa Simba Sven Vandenbroeck amemwanzishia benchi mchezaji huyo ambaye alianza kufanya mazoezi mepesi hivi karibuni.

Ilielezwa kwamba Mugalu na wenzake Meddie Kagere ambaye yupo kwao Kigali alikojiunga na timu ya taifa ya nchi hiyo Amavubi, Gerson Fraga ni majeruhi na watakosa mechi hii ya leo itakayoanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru na mechi zijazo.

Endapo Mugalu atapewa nafasi ya kucheza itamtengenezea ufiti wa mechi kutokana na majeraha ya nyonga yaliyokuwa yanamsumbua tangu alivyoumia kwenye mechi dhidi ya Prisons ambapo Simba walifungwa bao 1-0.

Ukiachana na Mugalu wachezaji wengine walio kwenye benchi la akiba ni, Aishi Manula, Gadiel Michael, Pascal Wawa, Mzamiru Yassin, Larry Bwalya na Miraji Athumani.

Katika hatua nyingine Sven ameamua kumpumzisha kabisa nyota wake Luis Jose katika mchezo huo wa Kagera Sugar kwa kuhofia kupata kadi ya njano ambayo itakuwa ya tatu kwake na itamfanya kukosa mechi ijayo dhidi ya Yanga itakayochezwa Novemba 7 mwaka huu.

Chanzo: Mwanaspoti