0

Msuva asepa na Kibabage Jadida

Msuva asepa na Kibabage Jadida

Wed, 11 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

Wakati mshambuliaji Simon Msuva akiachana na Difaa El Jadida ya Morocco na kujiunga na Wydad Casablanca pia ya nchini humo, Mtanzania mwingine anayeitumikia Jadida, Nickson Kibabage amejiunga na CA Youssoufia Berrechid inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja.

Kibabage ambaye ameitumikia Jadida kwa mwaka mmoja tangu alipojiunga nayo, Juni mwaka jana, usajili wake umekamilika jana lakini tofauti na Msuva, yeye atarejea Jadida mara baada ya mkataba huo wa mkopo kumalizika.

Mmoja wa wasimamizi wa Kibabage (20),  Abubakar Swabr alisema kuwa Kibabage ameridhia kujiunga na Youssouf Berrechid ili apate nafasi ya kutosha ya kucheza ambayo amekuwa haipati katika kikosi cha wakubwa cha Jadida.

"Hiyo timu iliyomsajili Kibabage, kacheza dhidi yao katika michezo mingi ya kirafiki ambayo ndio imefanya waridhike na kuvutiwa naye.

Ni hatua nzuri kwake kwani atapata muda wa kutosha wa kucheza kwani pale Jadida alikuwa anacheza zaidi katika kikosi cha vijana na timu ya wakubwa alikuwa anakaa benchi," alisema Swabr.

Kabla ya kujiunga na Jadida, Kibabage aliitumikia Mtibwa Sugar na kwa nyakati tfauti amechezea timu za taifa za vijana za Tanzania ile ya umri chini ya miaka 17 sambamba na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20.

Chanzo: Mwanaspoti