0

Messi kuungana na Guardiola

Messi kuungana na Guardiola

Thu, 3 Sep 2020 Source: HabariLeo

GWIJI la soka, Lionel Messi, amekubaliana mkataba wa miaka mitano na mmiliki wa Manchester City, imeelezwa.

Uamuzi wa mchezaji huyo kuondoka Barcelona umeunganishwa na mkataba huo ambao utamuwezesha mshindi huyo mara kadhaa wa Ballon d'Or kuwa mchezaji binafsi anayelipwa zaidi katika historia ya mchezo wa soka.

Mtandao wa Record Sport umesema Messi amekubali maslahi binafsi yenye thamani ya pauni milioni 623 (ambao ni sawa na Sh trilioni 1.9) katika kipindi cha mwaka mmoja akiajiriwa na City Football Group, kampuni inayomiliki klabu hiyo ya Ligi Kuu England.

Messi, ambaye Jumapili alianza kuifanyia mgomo klabu yake kwa kutokwenda katika vipimo vya covid-19 kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa La Liga na michuano ya kimataifa, anatarajiwa kutumia misimu mitatu Manchester City kabla ya kwenda katika klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani ya New York City FC.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, ambacho kinafahamu makubaliano hayo, Messi amepewa sehemu ya hisa katika kampuni hiyo ikiwa kama sehemu ya fidia.

Hata hivyo, kumekuwa na utata kuhusu makadirio ya hisa katika kampuni hiyo ya michezo ambayo City ilisema ilikuwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 4.8.

Messi, 33, imeelezwa ameamua kutua Man City badala ya kwenda kwa wapinzani wengine wa klabu hiyo wa Ulaya, kutokana na nia yake ya kutaka kucheza katika Ligi Kuu ya England akipigia hesabu mafanikio zaidi.

Mchezaji huyo anataka kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na tuzo ya saba ya Ballon d'Or wakati atakapoungana na kocha wake wa zamani Pep Guardiola ambaye alikuwa naye Barcelona miaka ya nyuma.

“Messi anafikiri Guardiola alimwezesha kucheza soka bora na anataka kurudi tena,” kilisema chanzo hicho ambacho kipo karibu na mchezaji huyo.

Katika kipindi kilichopita cha majira ya joto, Messi aliomba klabu hiyo kuongeza kasi ya kutaka kumrejesha Barcelona rafiki yake Neymar kutoka Paris Saint-Germain, PSG, kufanya kazi na wachezaji wenzake wazamani.

Chanzo: HabariLeo