0

Mchume ajitosa kuwania umakamu wa Rais TOC

Mchume ajitosa kuwania umakamu wa Rais TOC

Fri, 13 Nov 2020 Source: HabariLeo

MJUMBE wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Muharami Mchume amechukua fomu kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya umakamu wa Rais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Desemba 12 jijini Dodoma.

Mchume akizungumza na gazeti hili jana alisema baada ya kuitumia TOC kwa miaka takribani 12 kama mjumbe wa Kamati ya ya Utendaji, amepata uzoefu mkubwa na kuona anatosha kuchukua nafasi ya juu ili aendelee kuvitumikia vyama na mashirikisho mbalimbali ya michezo.

“Baada ya kuitumikia TOC kwa vipindi vitatu vya miaka minne minne kila kimoja, nimepata uzoefu mkubwa na sasa wakati umefika kwa mimi kuomba nafasi ya juu ili nivitumikie zaidi vyama,” alisema Mchume baada ya kuchukua fomu hiyo na kuahidi kuirejesha leo Ijumaa katika ofisi za TOC zilizopo Mwananyamala, Dar es Salaam.

Aliwataka wana michezo wengine kujitokeza kuwania ujumbe katika kamati hiyo.

Katibu Mku wa TOC, Filbert Bayi alisema zoezi la kuchukua fomu linakwenda taratibu na tayari Andrew Tandau, Noorlain Shariff na Juma Jambau wameshachukua fomu kutaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika kamati hiyo, wakati Alphonce Simbu, Restituta Joseph na Zakia Mrisho wanawania nafasi katika Kamisheni ya Wachezaji Tanzania (Kawata).

Alisema hadi sasa upande wa Zanzibar hakuna mtu aliyejitokeza kuchukua fomu na kuwahimiza watu kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fomu hizo kwani mwisho wa kuchukua na kurejesha ni Novemba 20, 2020.

Chanzo: HabariLeo