0

Mbio za Bima kusaidia watoto wenye saratani

Mbio za Bima kusaidia watoto wenye saratani

Tue, 8 Sep 2020 Source: HabariLeo

BENKI ya NMB inatarajia kukusanya zaidi ya Sh milioni 100 kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye saratani katika mbio za Bima Marathoni zilizopangwa kufanyika Septemba 12 jijini Dar es Salaam.

Fedha hizo zinatarajia kupatikana kupitia kwenye ada ya ushiriki wa mbio hiyo kwa upande wa Kilometa tano, ambazo zitashirikisha wadau mbalimbali waliojitokeza kushiriki katika mbio hizo zilizopangwa kuanzia Mlimani City, Dar es Salaam.

Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Wafanyabiashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema wanatarajia kushirikisha wanariadha 3,000 katika mbio hizo, ambazo zimeandaliwa na Kampuni ya The Africa Digital Banking Summit inayoongozwa na Baraka Mtavangu.

Mponzi alisema kuwa viingilio vyote vya mbio za kilometa 5 vitapelekwa kwenye hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya watoto hao.

Alisema kuwa mbio za kilometa 10 na 21 zitatumika zaidi kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa bima.

“Tunajisikia fahari sana kudhamini mashindano haya kwa ajili ya kusaidia jamii. Tunaomba wadau washiriki ili kufanikisha lengo au kuzidi lengo hilo,” alisema Mponzi.

Naye, Rehema Laiti ambaye ni Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili amewapongeza waandaji wa mbio hizo na zaidi Benki ya NMB kwa hatua hiyo na kuwataka watu wengine kuiga jambo hilo.

Mbali ya benki ya NMB, wadhamini wengine ni Kampuni za Bima za Alliance na UAP. Benki hiyo imetoa Sh milioni 35 kwa ajili ya udhamini wa mashindano hayo.

Chanzo: HabariLeo