0

Mayanga ateswa na ushindi Prisons

Mayanga ateswa na ushindi Prisons

Wed, 11 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

Kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Salum Mayanga amesema bado haridhishwi na ushindi mwembemba ambao timu hiyo inaupata katika michezo ya Ligi Kuu Bara, hivyo atatumia mapumziko ya kupisha michezo ya kimataifa kuisuka upya safu ya ushambuliaji.

Prisons yenye masikani yake jijini Mbeya imekuwa ikitumia Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa kama uwanja wake wa nyumbani, lakini imekuwa ikipata ushindi kwa shida katika kila mchezo wanaoibuka na ushindi.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, kocha huyo alisema atatumia kipindi hiki kufanyia kazi upungufu uliopo kwenye safu ya ushambuliaji ili timu hiyo ianze kuibuka na ushindi mnono katika michezo ijayo.

“Tunapata ushindi lakini bado ni mwembemba, hilo nimeliona, kwa hiyo tutatumia mapumziko haya ya michezo ya kimataifa kuinoa safu ya ushambuliaji ili iwe na makali,” alisema Mayanga.

Wadau wa soka mkoani Rukwa wamekuwa wakilalamika kuhusu ushindi kiduchu wa goli mojamoja wanaoupata Prisons katika michezo ya nyumbani, hivyo kutaka safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inolewe zaidi ili iwe na makali.

Vilevile, wadau wanadai Prisons yenye alama 15 ikiwa katika nafasi ya nane inatakiwa kutumia dirisha dogo lijalo la usajili linaloanza mwezi ujao kuongeza wachezaji kadhaa katika idara ya kiungo na ushambuliaji zinazoonekana kutokuwa na makali ya kutisha.

Chanzo: Mwanaspoti