0

Kuwaona Mwakinyo, Muargentina Sh3 milioni

Kuwaona Mwakinyo, Muargentina Sh3 milioni

Thu, 5 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By Imani Makongoro Dar es Salaam. Katika kulipa hadhi pambano la ubingwa wa mabara wa WBF na ule wa IBA la bondia Hassan Mwakinyo na Jose Carlos Paz wa Argentina, waandaaji wametangaza kiingilio cha juu kuwa Sh 3 Milioni wakati cha chini ni Sh 150,000.

Mwakinyo na Paz watazichapa Novemba 13 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki Dar es Salaam pambano ambalo litatanguliwa na mengine matatu ya mabondia wa Kenya, DR Congo, Zimbabwe, Zambia na Tanzania.

Mpinzani wa Mwakinyo atawasili nchini leo, ikiwa ni siku nane kabla ya kupanda ulingoni kuzichapa kwenye pambano hilo lililopewa jina la Dar Night Fight, ambalo Mwakinyo atakuwa akitetea ubingwa wa WBF, wakati huo huo akiwania mkanda wa IBA.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa alisema viingilio kwa pambano hilo vitaanzia Sh150,000 kwa eneo la kawaida na meza ya watu 10 itauzwa kwa Sh3 milioni.

“Kwenye meza kuu kutakuwa na huduma mbalimbali kuendana na hadhi ya kiingilio walicholipia,” alisema na kufafanua kuwa tiketi zitauzwa mtandaoni kupitia kampuni za Nilipe na Selcom.

Mpinzani wa Mwakinyo atawasili Dar es Salaam leo saa 4:30 usiku na ndege ya KLM akiwa na kocha wake, Alberto Ramon ambapo ameeleza sababu za kuwahi kuja nchini ni kutaka azoea hali ya hewa.

Chanzo: Mwanaspoti