0

Kipigo cha Yanga champanga Nizar

Kipigo cha Yanga champanga Nizar

Tue, 17 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By Thomas Ng’itu Dar es Salaam. Kocha wa African Lyon inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), Nizar Khalfan amesema mchezo wa kirafiki dhidi ya Yanga umempa taswira nzima ya kikosi chake.

Nizar licha ya kupoteza mchezo huo kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, alisema amepata somo zuri kutoka kwa mabingwa hao mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Unajua Yanga ina wachezaji wazuri na bora muda wote, hiki nikipimo tosha kwangu na kwa vijana wangu ambao wengi wao hawana uzoefu wa kucheza na timu kubwa kama Yanga,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Yanga na Taifa Stars.

Akizungumzia mchezo huo wa juzi, Nizar alisema katika kipindi cha kwanza wapinzani wao walishambulia mfululizo na kupata mabao yote matatu kwa dakika 30, jambo ambalo lilimfanya kubadili mbinu kipindi cha pili.

“Tulizidiwa, lakini niliwapa moyo wachezaji wangu na kuwatengenezea kujiamini na ndiyo maana kwenye kipindi cha pili tulicheza tofauti na ilivyokuwa kwenye kipindi cha kwanza ambacho tuliruhusu mabao yote.

“Lakini kama ambavyo ulikuwa (mchezo wa kirafiki), tumepata maandalizi mazuri katika kuendelea kwa Ligi Daraja la Kwanza ambayo tunashiriki,” aliongeza kocha huyo kijana.

Chanzo: Mwanaspoti