0

Kichuya ana hesabu kali Namungo

Kichuya ana hesabu kali Namungo

Thu, 17 Sep 2020 Source: Mwanaspoti

By OLIPA ASSASHIZA Kichuya ameonekana hana makali kama aliyokuwa nayo msimu wa 2016-2017 aliposajiliwa Simba akitokea Mtibwa Sugar, lakini kumbe jamaa ana hesabu zake katika Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na Namungo FC.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kichuya alisema soka ni mchezo wa hadharani unaochezwa kweupe, hivyo wale wanaodhani kafulia wasubiri waone mambo kwani anapambana kwa kadri anavyoweza ili kurejea kwenye kiwango ambacho atakuwa anatumika kwenye timu ya Taifa Stars.

Kichuya alisema anajiamini ana uwezo wa kubadili upepo kutoka kwenye ukimya wake na kuwa mchezaji mwenye ushindani katika ligi inayoendelea, akisisitiza anajifua kwa mazoezi makali ili kuhakikisha ndoto hiyo inakuwa kwenye vitendo.

“Ndio kwanza kumekucha, kadri ligi inavyoendelea kuchanganya ndivyo kila mchezaji anavyozidi kufanya vizuri, msimu huu kwangu nauchukulia kama wa kunirejesha kwenye kiwango changu,” alisema Kichuya na kuongeza;

“Soka ni biashara ambayo ipo wazi na kutazamwa na mamilioni ya watu duniani, hivyo natambua wazi kwamba kufanya vizuri kwangu ndiko kutanifanya nifikie malengo ninayoyataka yawe kwenye maisha yangu.”

Mwaka 2018 Simba ilimpeleka Kichuya kwa mkopo katika klabu ya Pharco ya Misri, tangu hapo jina lake lilianza kupotea taratibu masikioni mwa wadau, akaja akarejea mwakajana Msimbazi ambapo pia hakuwa na msimu mzuri.

Chanzo: Mwanaspoti