0

KCB yatoa Sh milioni 500 Ligi Kuu

KCB yatoa Sh milioni 500 Ligi Kuu

Thu, 17 Sep 2020 Source: HabariLeo

BENKI ya KCB imeingia mkataba wa udhamini wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara wenye thamani ya Sh milioni 500 kwa mwaka mmoja.

Huu ni msimu wa nne mfululizo benki hiyo inakuwa mmoja wa wadau muhimu wa kuunga mkono ligi hiyo na kuongeza thamani kutoka msimu mmoja kwenda mwingine.

Mkataba wa makubaliano ya udhamini huo ulisainiwa jana kati ya Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki kwa Wateja Wakubwa wa benki ya KCB Tanzania, Barry Chale na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Steven Mnguto ukishuhudiwa na viongozi wengine wa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa KCB, Chale alisema anawashukuru viongozi wa TFF kwa kuwapa nafasi ya kudhamini na kuendelea kuwa wadau wa maendeleo ya soka nchini.

“Udhamini wa msimu uliopita ulileta manufaa KCB, kwa Watanzania, wanamichezo na wanasoka wote hivyo, tunadhamini kwa kuwa sekta ya michezo ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi,” alisema.

Alisema kuna maeneo mengi wamekuwa wakidhamini kwa vipindi tofauti akitolea mfano mfungaji bora wa msimu uliopita, mchezo wa Ngao ya Jamii, kuchangia timu ya taifa ilivyoenda Afcon, Kombe la Shirikisho na Ndondo Cup.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa KCB, Christina Manyenye alisema wameendelea kuwa wadau wakiamini michezo ni sekta muhimu inayosaidia kukuza uchumi.

“Tumeona michezo ni mahali panapoendeleza uchumi, kuna ajira nyingi zinatolewa na pia kupitia udhamini huu kuna kodi inakatwa kwa hiyo tunachangia lakini pia, kuna vipaji vinaibuliwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPLB Mnguto aliishukuru KCB kwa kuunga mkono mpira wa Tanzania akisema zinasaidia klabu kutoa ajira kwa wachezaji.

“Tunapenda kuendelea na KCB kuunga mkono mpira wetu, mnarudisha kwa jamii na sifa inawarudia, hakuna mahali panakubalika kama kwenye mpira wa miguu, tunaamini hiki wanachokitoa ni kikubwa kinaongezea pale ambako tumepungukiwa,” alisema.

Chanzo: HabariLeo