0

John Bocco Apewa Silaha za Waarabu

John Bocco Apewa Silaha za Waarabu

Wed, 7 Apr 2021 Source: Global publishers

KOCHA Mkuu wa Simba raia wa Ufaransa, Didier Gomes Da Rosa, ameamua kumuweka kando Chris Mugalu na kumkabidhi majukumu mapya nahodha wa kikosi hicho, John Bocco kuhakikisha anaitungua Al Ahly na kurudi Dar wakiwa na pointi.

Aprili 9, mwaka huu, Simba itashuka katika Jiji la Cairo nchini Misri kupambana na Waarabu hao kwenye mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huo unafanyika ikiwa tayari Simba imejihakikishia kumaliza kinara wa Kundi A na kutinga robo fainali ya michuano hiyo sambamba na Al Ahly iliyopo nafasi ya pili.

Hivi sasa Simba ikiwa na pointi 13, imeizidi Al Ahly pointi tano kutokana na kukusanya nane, ambapo Gomes anataka kumaliza hatua hiyo akiwa hajapoteza mechi hata moja.

Gomes ameamua kuingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa, huku akipania kuweka rekodi hiyo ya kutopoteza mechi hatua ya makundi.Simba ambayo jioni ya leo Jumanne itaanza safari kuelekea nchini Misri baada ya mazoezi ya asubuhi yatakayofanyika Simba Mo Arena, Gomes amepanga kumtumia Bocco ambaye mpaka sasa hajacheza mechi hata moja hatua ya makundi kati ya tano walizocheza.Bocco anachukua nafasi ya Mugalu ambaye kwenye mechi hizo tano amecheza zote na kufunga mabao mawili.

Katika mazoezi ya jana Jumatatu asubuhi yaliyofanyika Simba Mo Arena, Dar na kushuhudiwa na Spoti Xtra, Gomes alimpa Bocco mazoezi maalum huku akimuweka kando Mugalu hali iliyotafsiriwa kwamba huenda akakaa benchi siku ya mechi hiyo.Gomes alifanya hivyo alipozigawa timu mbili zilizocheza mechi ya wenyewe kwa muda wa dakika kumi ambapo eneo la ushambuliaji kwenye kikosi kilichoonekana kuwa cha kazi, Bocco alianza, huku Mugalu akiishia nje.

WAANDISHI: MUSA MATEJA, LEEN ESSAU NA HAWA ABOUBAKHARI

Chanzo: Global publishers