0

JPM kutenga fedha kwa timu za taifa

JPM kutenga fedha kwa timu za taifa

Sat, 14 Nov 2020 Source: HabariLeo

RAIS John Magufuli amesema atatekeleza yale aliyoahidi kipindi cha kampeni katika sekta ya michezo na burudani ikiwemo kuanza kutenga fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kuzisaidia timu za taifa.

Magufuli alisema hayo jana mkoani Dodoma katika uzinduzi wa Bunge la 12 lililosheheni zaidi ya asilimia 60 ya Wabunge wapya waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa kitaifa mwishoni mwa mwezi uliopita.

“Tutaanza pia kutenga fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kuziandaa timu zetu za taifa na katika hilo napenda kutumia fursa hii kuitakia kheri Stars dhidi ya Tunisia na mwanamasumbwi Hassan Mwakinyo wanaocheza leo (jana),”alisema.

Stars ilitarajia kucheza na Tunisia jana usiku mechi ya kuwania kufuzu fainali za kombe la mataifa Afrika, Afcon na Mwakinyo alitarajiwa kupigana na bondia Jose Paz wa Argentina katika pambano la kuwania mkanda wa chama cha ngumi cha kimataifa (WBF).

Alisema hapendi kuona timu hizo zinashindwa kila wakati bali kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

Pia, alisema katika miaka mitano ijayo atakuza sekta ya sanaa na utamaduni ambayo inakua kwa kasi kubwa.

“Kama nilivyoahidi wakati wa kampeni tutakuza sekta hii hususani kwa kuimarisha masuala ya hatimiliki ili wasanii waweze kunufaika na kazi zao,”alisema na kuongeza kuwa anafarijika kuona kuna baadhi ya wasanii ambao ni wabunge miongoni mwao.

Alisema ataimarisha mfuko wa utamaduni na sanaa ili kuwasaidia wasanii ikiwemo kupata mafunzo na mikopo.

Chanzo: HabariLeo