0

Hatma ya Stars Chan kujulikana leo

Hatma ya Stars Chan kujulikana leo

Thu, 10 Sep 2020 Source: Mwanaspoti

By Charles AbelUshiriki wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) utajulikana leo Septemba 10, 2020.

Uamuzi wa kama mashindano hayo mwaka huu yatafanyika au la na pia kama nchi iliyopangwa kuyaandaa itabadilika au kubakia ileile, utafanywa na kamati ya utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) ambayo leo inaendesha kikao cha kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mchezo wa soka barani Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Caf, katika kikao hicho ambacho kitaendeshwa kwa njia ya mtandao kutokana na changamoto ya kufungwa kwa mipaka ya baadhi ya nchi kwa sababu ya tatizo la virusi vya Corona, agenda ya mashindano hayo ya Chan itakuwa  ni ya tano kujadiliwa katika kikao hicho.

Katika Agenda hiyo itakayojadili mashindano mbalimbali, fainali za Chan ndizo zitakuwa kipengele cha kwanza kujadiliwa na wajumbe na kitahusu mambo manne muhimu ambayo ni tarehe za mashindano ya Chan mwaka 2020, tarehe za Fainali za Chan mwaka 2022, mrejesho wa kanuni za kuwania kufuzu Chan na zile za fainali hizo pia iwapo kuna mabadiliko ya nchi mwenyeji na mwisho ni kuingiza kipengele cha nne katika kanuni ya kujitoa.

Hiyo ni miongoni mwa Agenda 12 ambazo kiujumla zitajadiliwa na wajumbe wa kamati ya utendaji ya Caf chini ya uongozi wa Rais Ahmad Ahmad nyingine zikiwa ni kukagua akidi, kupitisha maazimio ya kikao kilichopita, taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kikao cha dharura cha kamati ya utendaji, kikao cha kawaida, mashindano na taarifa ya mapato.

Mengine ni taarifa ya kamati ya sheria, taarifa ya rasilimali watu, taarifa ya miradi ya FIFA na Uefa, taarifa ya masoko, mengineyo na upangaji wa tarehe ya kikao kijacho.

Chanzo: Mwanaspoti