0

Cecafa U-20 kuchezwa Arusha

Cecafa U-20 kuchezwa Arusha

Wed, 18 Nov 2020 Source: HabariLeo

MICHUANO ya Vijana wa umri chini ya miaka 20 ya Baraza la mashirikisho ya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) inatarajiwa kufanyika katika viwanja viwili mkoani Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, jana Rais wa Cecafa, Wallace Karia alisema michuano hiyo itaanza kutimua vumbi Novemba 22 hadi Desemba 2, mwaka huu katika Uwanja wa Black Rhino akademi Karatu na Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Alisema nchi tisa zitashiriki ambazo ni wenyeji Tanzania, Somalia, Djibout, Burundi, Sudan Kusini, Uganda, Ethiopia, Kenya na Sudan.

“Tumepeleke michuano hii mikoani kueneza mchezo huu, michuano hii itafanyika lakini mashabiki hawataruhusiwa kuingia kutokana na mwongoza wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF),”alisema.

Alisema kabla ya kuanza michuano hiyo kila baada ya saa 48 wachezaji, viongozi na wote watakaohusika kwenye michuano hiyo ni lazima wapimwe corona.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Kidao Wilfred alisema anaishukuru Cecafa kwa kuwapa uenyeji na maandalizi yote yanakwenda vizuri.

Alisema kutakuwa na makundi matatu ambapo mawili yatatumia Uwanja wa Sheikh Abeid na kundi linaloongozwa na Tanzania litakuwa Karatu.

Kidao alisema kila kundi linatakiwa kutoa mshindi mmoja atakayeingia nusu fainali na kutakuwa na mshindwa bora mmoja.

Alisema timu zitakazofanya vizuri zitawakilisha Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwenye fainali za Afrika mwakani nchini Mauritius.

Tanzania imepangwa Kundi A sambamba na Somalia na Djibout, huku Kundi B likiwa na Sudan Kusini na Uganda na Kundi C lina Ethiopia, Kenya na Sudan.

Katika hatua nyingine Cecafa inatarajia kufanya Mkutano Mkuu mwezi ujao ambapo watatumia fursa ya kupanga kalenda kulingana na michuano kadhaa ya CAF na Cecafa.

Chanzo: HabariLeo