0

Bado mbili tu, Yanga ivunje rekodi

Mbili Pic Data Bado mbili tu, Yanga ivunje rekodi

Thu, 10 Jun 2021 Source: www.mwanaspoti.co.tz

YANGA inakaribia kuvunja rekodi yake ya mabao iliyofunga msimu uliopita licha ya wengi kubeza usajili wa washambuliaji wao ambao wamekuwa wakiinyima ushindi kwenye mechi nyingi msimu huu.

Mpaka sasa Yanga imefunga mabao 43 ikihitaji mawili tu katika mechi zake tano ilizobaki kuifikia rekodi yao ya msimu uliopita walipofunga mabao 45 katika mechi 38.

Washambuliaji wa timu hiyo wakiongozwa na Michael Sarpong, Yacouba Sogne, Fiston Abdulrazack, Ditram Nchimbi na Waziri Junior wamekuwa wakilaumiwa mara kwa mara kwa kukosa mabao mengi licha ya timu hiyo kutengeneza nafasi nyingi kwenye mechi zake hivyo kuinyima Yanga ushindi au hata inaposhinda inashinda kwa mabao machache.

Kwa upande wa washambuliaji, Yacouba pekee ndiye kinara wa mabao ndani ya timu hiyo akifunga mabao saba, Sarpong ana manne wakati Fiston, Nchimbi na Waziri wakiwa na bao moja kila mmoja.

Hata hivyo, licha ya washambuliaji wa timu hiyo kulegalega lakini mawinga kama Deus Kaseke mwenye mabao sita, Tuisila Kisinda (5) na mabeki wakiongozwa na Lamine Moro aliyefunga mabao manne ndio wameonekana kuibeba zaidi timu hiyo na kuifanya ikaribie kufikia rekodi yake ya mabao iliyofunga msimu uliopita.

Msimu iliopita ilimaliza ligi nafasi ya pili ikifunga mabao 45 katika mechi 38 wakati msimu huu bado mabao mawili tu kufikia rekodi hiyo.

Msimu huu ikicheza mechi 29, imefunga mabao 43 hivyo ikihitaji mawili au zaidi katika mechi zake tano ilizobakiwa nazo ili kuifikia au kuivunja rekodi yake ya msimu uliopita.

Kwa upande wa wapinzani wao Simba wanaweza ikawa rahisi kufikia rekodi yao ya mabao ya msimu uliopita walipofunga mabao 78 wakati msimu huu hadi sasa ikiwa imecheza mechi 26 imefunga 61 wakati Azam msimu uliopita ilifunga mabao 52, msimu huu hadi sasa ikicheza mechi 30 imefunga mabao 44.

ULINZI IKO MOTO

Msimu uliopita Yanga ilimaliza ligi ikiwa ni timu ya tatu kwa kuruhusu mabao machache (28) nyuma ya Simba iliyoruhusu mabao machache zaidi (21) na Azam (26). Hata hivyo, msimu huu Yanga imeonekana imara zaidi kwenye safu ya ulinzi kwani licha ya wapinzani wao wakubwa Simba wanaongoza kwa kuruhusu mabao machache (11) lakini inafuatia ikiwa imeruhusu mabao 17 na dalili zinaonyesha wanaweza kuendelea kukomaa na kumaliza msimu kwa mabao machache zaidi ya waliyofungwa msimu uliopita.

Kocha wa zamani wa Azam, Ndanda na Lipuli, Meja Mstaafu Abdul Mingange alisema “Kweli washambuliaji hawajaitendea haki timu hiyo kwani hawako katika kiwango kilichotarajiwa na wengi wakati wanasajiliwa tofauti na Simba ambao wako vizuri kwa upande wa ufungaji wa mabao kwenye mechi zao na hiyo imetokana na kukaa kwa pamoja muda mrefu hivyo wanaelewana aina yao ya uchezaji.

“Hata hivyo Yanga wamejitahidi kwa sababu wachezaji wengine katika nafasi tofauti tofauti wamekuwa wakifunga na kuibeba timu hiyo na ndio maana wanakaribia kufikia rekodi yao ya mabao ya msimu uliopita.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz