0

BMT yawaita RT kujadili uchaguzi

BMT yawaita RT kujadili uchaguzi

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) litawaita viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ili kujadili suala la marekebisho ya Katiba na Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo.

Awali, Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya RT ilikabidhi kazi yake kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ambaye naye alikabidhi kwa uongozi wa RT ili kuifanyia kazi.

Hata hivyo, RT pamoja na kukabidhiwa marekebisho hayo, kamati yao ya utendaji iimeshindwa kukutana kujadili suala hilo kwa madai kuwa siku waliyopanga kukutana wajumbe wa Kamati ya Katiba wasio wajumbe wa RT hawakutokea katika kikao hicho.

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha akizungumza kwa njia simu jana alisema wamebaini ukimya wa RT katika suala hilo na watakutana nao baada ya mbio za Dodoma Marathon zitakazofanyika Jumapili.

“Tumewapa muda wamalize mbio zao walizoandaa Dodoma na baada ya mbio hizo watakutana na ndipo watajua utaratibu mzima wa marekebisho ya Katiba pamoja na mkutano wa uchaguzi mkuu.”

“Tutakutana baada ya RT kumaliza mbio zao za Dodoma na hapo ndipo tutajua mkutano mkuu utafanyika lini na wapi,” alisema Msitha.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka RT, baadhi ya mambo yaliyopendekezwa kubadilishwa na Kamati ya Katiba ni kupunguza idadi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji, kutopiga kura kamati inayomaliza muda wake na kila mkoa kuwa na mwakilishi mmoja katika mkutano mkuu badala ya wajumbe watatu ili kupunguza gharama.

Chanzo: HabariLeo