0

Azam waziombea sare Yanga na Simba

Azam waziombea sare Yanga na Simba

Fri, 6 Nov 2020 Source: Mwanaspoti

By CHARLES ABELKOCHA wa Azam FC, Aristica Cioaba amesema kuwa timu yake inatamani Simba na Yanga zitoke sare katika mchezo wao wa Ligi Kuu utakaozikutanisha kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Kocha huyo aliliambia Mwanaspoti Online kuwa matokeo ya sare katika mchezo huo yatakuwa na maana kubwa kwa timu yake tofauti na iwapo timu moja kati ya Yanga au Simba ikiibuka na ushindi.

"Hii ni mechi kubwa na zinakutana timu kubwa nchini kama ilivyo Azam hivyo nategemea watuonyeshe soka safi na la kuvutia linaloendana na hadhi yao kwani timu zote ziko vizuri.

"Binafsi naamini timu yoyote inaweza kupata ushindi lakini ukiniuliza aina ya matokeo ambayo ningetamani kuona yakitokea basi nitasema yawe sare," amesema Cioaba.

Kocha huyo amesema kuwa ikitokea timu mojawapo ikafungwa, bado haitokuwa na madhara yoyote kwa Azam FC kwani wao wamejipanga kuhakikisha wanakusanya pointi nyingi kadri iwezekanavyo pasipo kutegemea matokeo ya Simba na Yanga.

"Sisi tuna malengo yetu na hatupaswi kutegemea timu nyingine ipate matokeo fulani ndio tunufaike. Tunatakiwa kupata ushindi katika mechi zetu wenyewe na hilo ndilo tunalitilia mkazo kwa sasa na sio vinginevyo," amesema Cioaba.

Chanzo: Mwanaspoti