0

Azam kuifuata Mbeya City kesho

Azam kuifuata Mbeya City kesho

Thu, 17 Sep 2020 Source: Mwanaspoti

By Clezencia TryphoneMsafara wa watu 35 wakiwemo wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi la klabu ya Azam FC unatarajia kuondoka kesho mchana kwa basi kuwafuata Mbeya City katika mchezo ujao.

Azam FC atakuwa mgeni wa Mbeya City katika mchezo wa raundi ya tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

 Mbeya City ilianza vibaya ligi kwa kukubali kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya KMC na mchezo uliofuata ikikumbana na kipigo kingine cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga  huku Azam FC wenyewe wakishinda michezo yao yote miwili dhidi ya Polisi Tanzania kwa bao 1-0 na  dhidi ya Coastal Union kwa mabao 2-0.

Mkuu wa Idara ya Habari ya Klabu hiyo Thabit Zakaria amesema kila mchezo kwao ni fainali kwani mwaka huu wana mipango mikubwa katika Ligi na Kombe la FA.

Amesema michezo ya awali walitumia vyema uwanja wa nyumbani na sasa wanaenda ugenini watajitahidi kuhakikisha wanapata matokeo japokuwa kila mchezo kwao ni fainali.

"Kesho mchana tunaondoka kwenda Mbeya Msafara mzima utakuwa na watu 35, Wachezaji 23, viongozi wa benchi la ufundi tisa pamoja na viongozi wengine, tunaimani na kikosi chetu tutaenda kufanya vizuri japokuwa hakuna mchezo mwepesi katika ligi kila timu imejiandaa,"amesema.

Chanzo: Mwanaspoti