0

Amavubi yaifuata Cape Verde kwao

Amavubi yaifuata Cape Verde kwao

Tue, 10 Nov 2020 Source: HabariLeo

TIMU ya taifa ya soka ya Rwanda, Amavubi, ilitarajia kuondoka nchini jana kwa ndege ndogo ya RwandaAir kwenda Cape Verde kwa ajili ya mchezo wa kuifuzu wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon 2021, Novemba 12.

Cape Verde wataikaribisha Rwanda katika mchezo wa kwanza utakaofanyika Alhamisi kabla ya vijana wa kocha Vincent Mashami kuwa wenyeji katika mchezo utakaofanyika Novemba 17.

Timu hizo ziko katika Kundi F katika michuano hiyo ya kusaka nafasi ya kucheza fainali za Afcon 2021 zitakazofanyika Cameroon.

Wakati Cape Verde na Rwanda bado hazijashinda baada ya kucheza mechi mbili kila moja, mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa Mashami na vijana wake wakati wakiangalia kupata pointi moja baada ya kupoteza mechi awali dhidi ya Msumbiji na Cameroon.

Ushindi wa nyumbani kwa Cape Verde utawainua hadi pointi tano baada ya kutoka sare dhidi ya Msumbiji na Cameroon Novemba mwaka jana.

Kocha Mkuu Mashami juzi Jumapili alitangaza kikosi cha wachezaji 23 ambacho kitakabiliana na Cape Verde na msafara huo ulitembelewa na Waziri wa Michezo, Aurore Mimosa Munyangaju.

Kikosi kamili:

Makipa: Yves Kimenyi (Kiyovu), Olivier Kwizera (Rayon) na Eric Ndayishimiye (AS Kigali).

Mabeki: Thierry Manzi (APR), Abdul Rwatubyaye (Switchbacks, Marekani), Fitina Ombolenga (APR), Emmanuel Imanishimwe (APR), Eric Rutanga (Polisi), Ange Mutsinzi (APR), Aimable Nsabimana (Polisi) na Hervé Rugwiro (Rayon).

Viungo: Djihad Bizimana (Beveren, Belgium), Yannick Mukunzi (Sandvikens, Sweden), Haruna Niyonzima (Yanga, Tanzania), Kevin Muhire (El Gaish, Misiri), Ally Niyonzima (Azam, Tanzania), Dominique-Savio Nshuti (Polisi), Djabel Manishimwe (APR) na Steve Rubanguka (Karaiskakis, Ugiriki).

Washambuliaji: Meddie Kagere (Simba, Tanzania), Jacques Tuyisenge (APR), Muhadjiri Hakizimana (AS Kigali) na Osée Iyabivuze (Polisi).

Wakati huohuio, kiungo anayecheza soka Misri Kevin Muhire alitua nchini na kujiunga na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Cape Verde.

Mchezaji anayecheza soka huko Armenia, Salomon Nirisarike ameondolewa katika kikosi hicho baada ya wiki iliyopita kukutwa na maambukizi ya covid-19.

Kikosi cha Amavubi kinashika mkia katika kundi F baada ya kutokuwa na pointi hata moja licha ya kushuka dimbani mara tatu, wakati Cape Verde wako katika nafasi ya tatu wakiwa na poiti mbili.

Cameroon ambao ni wenyeji wa fainali za Afcon 2020, wanashikilia uongozi wa kundi hilo pamoja na Msumbuji kutokana na kila moja kuwa na pointi nne.

Mwingine aliyejiunga na kambi hiyo ni Ally Niyonzima kiungo mwingine wa kimataifa wa Rwanda anayecheza soka la kimataifa Tanzania akiwa na mabingwa wa zamani wa Kombe la Kagame Azam FC.

Chanzo: HabariLeo