0
Menu
Infos

Watakaosababisha ajali kuadhibiwa papo hapo

Watakaosababisha ajali kuadhibiwa papo hapo

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri Barabarani inakusudia kuanzisha adhabu za papo kwa papo kwa madereva kama sehemu ya mikakati ya kudhibiti ajali za barabarani ambazo husababisha vifo na ulemavu kwa wananchi.

Akizungumza mjini hapa jana, Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Mohamed Simba alisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kuwapo kwa matukio mengi ya ajali za barabarani zinazosababishwa na uzembe na kusababisha vifo vya wananchi na wengine kupata ulemavu wa kudumu.

Alisema serikali ya Zanzibar imeunda mamlaka mpya ya kudhibiti usafiri barabarani chini ya sheria namba 10 ya mwaka 2019 ambayo itakuja na mikakati ya kudhibiti ajali hizo.

“Mchakato wa kuanzishwa kwa adhabu za papo kwa papo ulikuwa unasubiri utekelezaji wake ikiwamo kuundiwa kanuni zitakazofanyakazi, lakini sheria mpya ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Barabarani imesababisha mchakato huo kuanzishwa tena.”

“Mamlaka hiyo imeanza kazi takriban miezi minne sasa kwa sheria namba 10 ya mwaka 2019 ambayo imefuta sheria ya idara ya usafiri na leseni ya mwaka 2003, sasa tumejipanga kuja na sheria ambazo zitasaidia kudhibiti ajali za barabarani,” alisema.

Simba alisema lengo kubwa la mamlaka hiyo ni kuleta ufanisi katika huduma za usafiri pamoja na kuweka kanuni na sheria zitakazofanya kazi kwa maslahi ya wananchi na kupunguza wimbi la ajali nchini.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano wanakusudia kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule mbalimbali Unguja na Pemba, pamoja na kuingiza katika mitaala somo la usalama barabarani.

“Hiyo ni sehemu ya mikakati yetu kuona kwamba wananchi wote wanafahamu sheria za usalama barabarani wakiwemo wanafunzi ambao ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa barabara,” alisema.

Chanzo: HabariLeo