0
Menu
Infos

Wataka mjadala wa kitaifa kukomesha mimba za utotoni

Wataka mjadala wa kitaifa kukomesha mimba za utotoni

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

WADAU wa elimu mkoani Kigoma wamesema mjadala wa kitaifa kwa watunga sheria unahitajika ili kulipatia ufumbuzi tatizo la wazazi, wanafunzi na watuhumiwa wanaowapa ujauzito wanafunzi ambao wamekuwa wakishirikiana na kuharibu ushahidi.

Wadau hao wamesema jambo hilo linasababisha watuhumiwa wa mimba za wanafunzi kushindwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hayo yalibainika katika mahojiano maalumu yaliyofanywa na HabariLEO kwa wadau mbalimbali mjini Kigoma na kueleza kuwa kuharibu ushahidi kwa kesi za mimba za wanafunzi limeanza kuwa tatizo ambalo linashindwa kupunguza kama siyo kuondoa kabisa tatizo hilo.

Mkuu wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, Doris Sweke alisema licha ya jitihada kubwa wanayofanya kufuatilia na kuwakamata watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi na baadaye kesi kufikishwa mahakamani, lakini kesi hizo zimekuwa hazina mwisho mzuri.

Hiyo inasababisha watuhumiwa kutopata adhabu kutokana na mwanafunzi na wazazi wake kushirikiana na mtuhumiwa ambapo mwathirika hufundishwa kumkana mtuhumiwa.

Naye Mratibu wa Asasi ya Maendeleo ya Wanawake Kigoma (KIWODE), Sophia Nassibu alisema amekuwa akijihusisha na masuala mbalimbali ya elimu kwa wasichana kupitia ufadhili kwa Asasi ya Hakielimu na huko wanakumbana na changamoto kubwa ya mimba za wanafunzi.

"Tunapofuatilia tumegundua kuwa tangu adhabu ya kifungo iongezwe kutoka miaka saba kuwa 30 pande tatu za mimba za wanafunzi zimekuwa zikishirikiana kuharibu ushahidi ili kumbana mtuhumiwa kuweza kumuhudumia mwanafunzi na mtoto wake, maana kama amepoteza masomo akibaki nyumbani utakuwa mzigo wa wazazi, hii ni changamoto kubwa,"alisema.

Taarifa kutoka Idara ya Elimu ya Sekretariet ya Mkoa Kigoma, inaonesha kuwa kwa miaka miwili 2019 na mwaka huu jumla ya wanafunzi 50 walishindwa kumaliza masomo yao kwa sababu ya ujauzito.

Ofisa Elimu wa Mkoa Kigoma, Paulina Ndigeza alisema kutokana na kuendelea kwa takwimu za mimba za wanafunzi wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanzisha ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule mbalimbali za sekondari mkoani humo.

"Pamoja na hilo tumekuwa tukichukua hatua kwa kushirikiana na wazazi kuhakikisha kesi zinafikishwa mahakamani na watuhumiwa wanaadhibiwa ili iwe fundisho, bahati mbaya kesi ikishafika mahakamani tunaachia muhimili wa mahakama ufanye kazi yake, lakini taarifa za matokeo ya kesi tunazopata sio nzuri kesi nyingi haziishi vizuri,"alisema.

Akizungumzia tatizo hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigoma, Keneth Mutembei alisema ushahidi usiotia shaka ndiyo pekee ambao unampa nafasi hakimu kutengeneza hukumu yake dhidi ya mtuhumiwa.

Mutembei alisema mwanafunzi ambaye ndiye shahidi wa kwanza na anayemjua mtuhumiwa anapaswa aieleze mahakama nani anahusika na ujauzito huo, hivyo anapokana kuwa mtuhumiwa aliyefikishwa mbele ya mahakama siyo muhusika, hakimu huwezi kutoa hukumu kwa uonevu.

Chanzo: HabariLeo