0
Menu
Infos

Wasomi: Alichosema JPM kinahusu wateule wote

Wasomi: Alichosema JPM kinahusu wateule wote

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

WASOMI nchini wamesema angalizo la Rais John Magufuli kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu kubaki au kuondolewa kwenye nafasi hiyo linawahusu wateule wote serikalini.

Baada ya Rais Magufuli kumuapisha Majaliwa Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma aendelee kuwa Waziri Mkuu alimueleza kuwa kuteuliwa kwake hakuna maana kuwa lazima awe na madaraka hayo kwa miaka mingine mitano.

Kwa nyakati tofauti wasomi hao walilieleza HabariLEO kuwa kauli ya Magufuli pia inamtaka Majaliwa aongeze usimamizi kwa viongozi walio chini yake ili kuongeza kasi ya maendeleo.

Magufuli alisema, Majaliwa ni mchapakazi, msikivu, anafahamu uongozi na malengo ya Serikali na ndio maana hakupata shida kumteua lakini haina maana kuwa lazima awe Waziri Mkuu kwa miaka mingine mitano.

“Na ndio maana nilipomteua wakati anafanya hivi machozi yanatokatoka na mimi nilikuwa nalengwa machozi, lakini nikasema; you deserve (unastahili), lakini no guarantee, hii ndio observation (taswira) ambayo mnatakiwa kuichukua ina-depend (inategemea) na perfomarnce (utendaji) ya kazi” alisema.

Profesa Mshiriki wa Shule Kuu ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Razack Lokina, alisema kauli ya Rais Magufuli ilikuwa ni ukumbusho kwa watendaji kwamba amewachagua kwa kuwa anafahamu utendaji wao hivyo wasibweteke.

“Ilikuwa ni angalizo (wakeup call) kwa watendaji wa chini yake kuwa anafahamu utendaji kazi wao, amewachagua kwa nafasi hiyo kwa kuwa anafahamu ataiweza, hivyo wasibweteke kwani ana mamlaka pia ya kutengua akiona mambo hayaendi kama anavyotaka’’alisema Profesa Lokina.

Alisema kwa angalizo hilo pia, ni wazi kwamba anampa salamu Waziri Mkuu kuzifikisha pia kwa mawaziri wote watakaoteuliwa kwani kiutendaji, Waziri Majaliwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali.

“Kila mmoja amesikia watatekeleza, lazima wajue kwamba serikali hiyo sio ya kulala ni kufanya kazi kama dira ya Rais Magufuli inavyoeleza,’’alisema Profesa Lokina.

Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam, Dk Lazaro Swai, alisema kauli ya Rais Magufuli ni maelekezo kwa walio chini yake kuhakikisha wanafanya kazi kwa kiwango cha juu.

“Kauli ya Rais Magufuli kwenda kwa Waziri Mkuu ni kuonesha dira na uelekeo wa serikali anayoiongoza, hivyo wote walio chini yake wanatakiwa kwenda kwa kufuata dira hiyo, ni jambo la kawaida kwa kiongozi kutoa mwelekeo ya mambo anayotaka yashughulikiwe,’’alisema Dk Swai.

Alisema kiutawala Waziri Mkuu ndiye kioo cha serikali na anawajibika katika utekelezaji wa ahadi kwa wananchi hivyo ni lazima aweke msisitizo ili watendaji wote kwa nafasi zao watimize wajibu wao.

Alisema kauli ya Magufuli ina tija na manufaa makubwa kwa watendaji kwa kuwa itasaidia kuwaongezea ari na ubunufu katika utendaji kazi hivyo kero za wananchi zitapatiwa ufumbuzi.

“Hii kauli itabadilisha utendaji wa mawaziri wote, kwa maana tumeshuhudia sasa na wengi wameshamsoma Rais ni mtu wa namna gani, anapenda nini katika kuwajibika, hivyo kila mmoja atahakikisha kwa nafasi yake anatekeleza wajibu wake’’alisema Dk Swai.

Mwanadiplomasia na mchambuzi wa uchumi, Dk Watengere Kitojo alisema kauli ya Rais Magufuli itasaidia watendaji wengi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuwa wabunifu zaidi kwa sababu wameshafahamu dira ya Rais na maono yake kwa nchi.

“Nilifurahi kusikia kauli ile ya Rais Magufuli, Watanzania tunafanya kazi kwa mazoea, lazima tuamshwe, kauli ile itawafanya watendaji kuwa wabunifu, Waziri Mkuu pale alikuwa akielezwa kuwa amekuwa naye kipindi cha kwanza, anafahamu utendaji kazi wake hivyo lazima afanye kwa zaidi kipindi hiki,’’ alisema Dk Kitojo.

Alisema mbali na Waziri Mkuu, Rais Magufuli ameshuhudia kero za wananchi katika maeneo tofauti ya nchi wakati wa kampeni na kubaini kuwa bado kuna watendaji wasiotimiza wajibu wapo hadi kero zinamfikia yeye wakati zilipaswa zipatiwe ufumbuzi na wasaidizi wake.

“Ni lazima watendaji waamke wafanya kazi kwa kiwango cha juu zaidi, Rais Magufuli amezunguka maeneo tofauti ya nchi, amebaini kuna kero nyingi zilipaswa kushughulikiwa na wateule wake na sio yeye, sasa anawatahadharisha mapema wawajibike kwenye nafasi zao,’’alisema Dk Kitojo.

Chanzo: HabariLeo