0
Menu
Infos

Wapya watawala serikali ya Dk Mwinyi

Wapya watawala serikali ya Dk Mwinyi

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametangaza Baraza la Mawaziri lenye wizara 15 zikiwemo nne zitakazokuwa chini ya ofisi yake.

Wizara mbili kati ya hizo, hazina mawaziri, kaingiza sura mpya 9 wengi wakiwa ni vijana wanaoongoza wizara kwa mara ya kwanza.

Wizara ambazo hakuteua mawaziri ni Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.

“Hizo wizara mbili bado sijateua mawaziri wake kwa sababu nasubiri majina kutoka kwa chama cha ACT-Wazalendo ambacho kimeshika nafasi ya pili katika wingi wa kura kwa mujibu wa maridhiano ya kisiasa,” alisema Dk Mwinyi.

Katika baraza hilo, ni mawaziri 4 tu waliokuwa katika baraza lililopita akiwemo Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman.

Suleiman amekuwa katika Baraza la Mawaziri kwa miaka 20 tangu kipindi cha Rais mstaafu, Amani Abeid Karume.

Wakati huo aliongoza Wizara ya Elimu kwa vipindi viwili hadi Rais mstaafu, Dk Ali Mohammed Shein. Riziki Pembe Juma amerudi katika baraza hilo lakini safari hii kupitia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Wengine waliorudi, ni Dk Khalid Salum Mohamed mwakilishi wa Jimbo la Donge ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera na Uratibu wa Baraza la Wawakilishi.

Salum alipata kuwa Waziri wa Fedha katika awamu iliopita kuanzia 2015-2019 kabla ya uteuzi wake kutenguliwa.

Pia kiongozi huyo alipata kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa muda wa miaka mitano akishughulikia masuala ya Uratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Simai Mohamed amechaguliwa kuwa Waziri wa Elimu. Katika serikali iliyopita, alikuwa Naibu Waziri wa Elimu.

Sura mpya katika baraza hilo waliofanikiwa kushika nafasi za uwaziri ni 9 akiwemo Jamali Kassim Ali, mwakilishi wa Jimbo la Magomeni ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi Rais Fedha na Mipango.

Kabla ya uteuzi huo kwa muda wa miaka mitano alikuwa Mbunge wa Jimbo la Magomeni na amepata kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) akiwa na elimu ya juu katika masuala ya fedha na katika nyakati tofauti alipata kuwa Mkurugenzi wa Fedha Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uchumi na Uwekezaji ni Mudrik Ramadhan Soraga ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Bububu.

Kabla ya hapo alikuwa Ofisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kikanda na baadaye kuteuliwa kuwa Balozi Mdogo nchini Comoro.

Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ ni Masoud Ali Mohamed, mwakilishi wa Jimbo la Ole ambaye alikuwa Ofisa Mdhamini Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Pemba.

Katika sura mpya nyingine ni Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji Maji, Maliasili na Mifugo, Dk Soud Nahoda Hassan ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Paje.

Nahoda ana elimu ya juu ya uzamivu katika masuala ya kilimo na alikuwa Mkuu wa Chuo cha Kilimo Kizimbani Unguja ambacho kwa sasa kimehamishiwa na kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA).

Tabia Maulid Mwita ambaye ni mwakilishi wa kuteuliwa na Rais akiwa Makamu Mwenyekiti wa (UVCCM) ameteuliwa kuongoza Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.

Miongoni mwa sura mpya ni Leila Mussa kutoka viti maalumu ameteuliwa kuongoza Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, wakati Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ikishikiliwa na Rahma Kassim Ali kutoka Viti Maalumu Wanawake.

Kabla ya uteuzi huo, Rahma alikuwa Mkurugenzi wa Usajili na Matukio ya Kijamii katika Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalumu SMZ.

Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi ameteuliwa Abdalla Hussein Kombo ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Mkoani Pemba na kabla ya uteuzi mpya alikuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA).

Dk Mwinyi amemteua mwakilishi wa Jimbo la Chonga, Pemba Suleiman Masoud Makame kuwa Waziri wa Maji, Nishati.

Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mwanasheria wa Wizara ya Mawasiliano na Usafirishaji akiwa Mdhamini Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini (ZMA) kwa upande wa Pemba.

Katika baraza hilo mawaziri ambao hawakurudi katika Serikali ya Awamu ya Nane ingawa wameibuka na ushindi katika majimbo ya uchaguzi ni Issa Haji Ussi mwakilishi wa Jimbo la Chwaka ambaye aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Mwingine ni Haji Omar Kheir ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akiwa mwakilishi wa jimbo la Tumbatu.

Katika uteuzi huo wapo wanawake wanne ambao wote ni mawaziri kamili. Dk Mwinyi hajateua manaibu waziri hadi mahitajiti yatakapojitokeza.

Chanzo: HabariLeo