0
Menu
Infos

Wakulima, wafugaji washauriwa kilimo mseto

Wakulima, wafugaji washauriwa kilimo mseto

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amewataka wakulima na wafugaji nchini kutumia kilimo mseto ili kuongeza uhakika wa chakula na kipato.

Alitoa wito huo jana wakati akizindua maonesho ya siku tatu ya kilimo mseto mkoa wa Mara yanayofanyika mjini Musoma.

Maonesho hayo yanawashirikisha wakulima, wafugaji na wavuvi chini ya uratibu wa shirika la Vi Agroforestry pamoja na taasisi za serikali na wadau wa sekta ya kilimo.

Kusaya alisema wizara hiyo inaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wakulima kupata elimu na teknolojia bora ili kilimo kiwe na tija na kukuza uchumi, hivyo uwapo wa maonesho hayo una mchango mkubwa kwa wakulima.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Kalorine Mthapula alisema mkoa huo unaendelea kuhamasisha wakulima kujikita kwenye shughuli za kilimo na kwamba kupitia maonesho ya kilimo mseto wana uhakika uchumi wa mkoa utaendelea kukua.

Alisema pamoja na maonesho hayo, mkoa huo umeanzisha viwanja maalumu vya Nanenane vinavyojulikana kama Mama Maria Nyerere wilayani Butiama kwa lengo la kutumika kufanya maonesho ya kilimo, mifugo na uvuvi ili elimu iwafikie wananchi wengi kwa karibu.

"Kila tarehe 15 Septemba mkoa wa Mara huadhimisha siku iitwayo Mara Day kwa lengo la kuhamasisha kilimo, ufugaji na uvuvi kupitia viwanja vyetu vya Nanenane vya Mama Maria Nyerere huko Butiama ambapo pia siku hiyo hutumika kuhamasisha uhifadhi endelevu la Bonde la Mto Mara," alisema.

Mkurugenzi wa Shirika la Vi Agroforetry, Thadeus Mbowe alisema maonesho ya mwaka huu yamesheheni teknolojia mbalimbali za kilimo mseto kupitia washirika wenza wakiwamo watafiti na wataalamu wa kilimo wanaotoa elimu kwa wananchi.

Kauli mbiu ya maonesho ya kilimo mseto mwaka huu inasema ‘Kilimo mseto kwa usalama wa chakula na kipato.’

Chanzo: HabariLeo