0
Menu
Infos

Wafanikiwa kusitisha ndoa ya binti miaka 15

Wafanikiwa kusitisha ndoa ya binti miaka 15

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

VIONGOZI wa Kata ya Mpwayungu kwa kushirikiana na wananchi wamefanikiwa kusitisha ndoa ya binti wa miaka 15 iliyokuwa ikifungwa usiku.

Tukio hilo limetokea katika Kitongoji cha Muungano Kata ya Mpwayungu Wilaya ya Chamwino mkoani hapa.

Akizungumzia tukio hilo lililotokea hivi karibuni, Mtendaji wa Kata ya Mpwayungu, Azania Anderson alisema siku ya tukio walipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kuna msichana mdogo anataka kuozwa.

Alisema baada ya kupewa taarifa hizo, walilazimika kuvamia eneo la tukio saa 4:00 usiku wakati sherehe za ndoa za kimila zikiendelea.

“Tulivamia eneo la tukio saa 4:00 usiku wakati sherehe ya ndoa ya kimila zikiendelea, kulikuwa na giza sana, hata hivyo bwana harusi na watu aliokuja nao walifanikiwa kukimbia.

“Hata hivyo, tulifanikiwa kumkamata, mama wa binti na baba wa binti, Juma Mathayo,”alifafanua.

Anderson alisema bwana harusi aliyetaka kumuoa binti huyo aliyekuwa amemaliza darasa la saba mwaka jana anafahamika kwa jina la Stephano Malugu mkazi wa kijiji cha Ng’ambako.

Alisema wazazi wa binti walipelekwa katika kituo cha polisi Chamwino na kupata dhamana na juhudi za kuwatafuta muoaji na wazazi wake zinaendelea.

Mmoja wa wakazi wa Mpwayungu, Festo Manjechi alisema baada ya kupata taarifa ya uwepo wa doa hiyo ambayo ilikuwa ifanyike kitongoji cha Muungano waliamua kupeleka taarifa kwa mtendaji kata.

“Tulivyopata taarifa ya kuwapo kwa tukio la ndoa ya utotoni, tulitoa taarifa kwa viongozi wa kata ambao siku ya tukio walivamia ingawa bwana harusi na wazazi wake walikimbia,”alisema.

Alisema baadaye taarifa ilitolewa kituo cha polisi cha kata na ndipo watuhumiwa ambao ni wazazi wa binti walitiwa mbaroni.

Alisema wananchi wamekuwa na uelewa na sasa wanapinga ndoa za utotoni kufanyika katika maeneo yao.

“Kumekuwa na mwamako mkubwa kwa wananchi katika kupambana na ndoa za utotoni katika jamii yetu, hivyo kutoa taarifa pindi matukio yanapotokea ni jambo la kutia moyo kuwa jamii inapinga ndoa za utotoni,”alisema.

Kwa upande wa Mratibu wa Dawati la Mtoto kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai alisema wamepata taarifa juu ya uwepo wa tukio hilo na kwa sasa wanafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.

Naye Mratibu wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Women Wake Up (WOWAP), Nasra Suleiman alisema walipata taarifa juu ya uwepo wa tukio hilo kutoka kwa wananchi na waelimisha rika wa mradi wa kutokomeza ukatili kwa kupunguza mimba na ndoa za utotoni wanaoutekeleza katika kata hiyo.

“Kwa sasa wananchi wanaona umuhimu wa kutoa taarifa na mara kadhaa wamekuwa wakivunja ndoa za utotoni zisifungwe, haya ni matunda ya kazi tunayoifanya,”alisema.

Chanzo: HabariLeo