0
Menu
Infos

WAWILI WAKUTWA WAKIWA WAMESHAFARIKI DUNIA

WAWILI WAKUTWA WAKIWA WAMESHAFARIKI DUNIA

Sat, 21 Nov 2020 Source: Zanzibar 24

Vijana wawili wamekutwa wakiwa tayari wameshafariki dunia katika bwawa la mradi wa umwagiliaji maji uliopo Kinyasini kisongoni baada ya kutoonekana nyumbani kwao tangu siku ya Jumatano ya wiki hii.

Vijana hao waliofahamika kwa majina ya Khamisi  Rajab Mohammed na Nassor Kibwana Khamisi  wenye umri wa miaka 25 wote wakaazi wa  shehiya ya Chaani kubwa  wamekutwa asubuhi ya jana katika eneo hilo wakiwa tayari wameshafariki dunia.

Akizungumza na Zanzibar24 sheha wa shehiya ya chaani kubwa  Bw: Abdul-ghafur Ibrahim Ussi amethibitisha kuwa marehemu hao ni wakaazi wa shehiya yake ambao  walikuwa  wanajihusisha na tabia ya uvutaji wa dawa za kulevya pamoja na ulevi .

Amefahamisha kuwa alipokea taarifa ya kupotea kwa vijana hao kutoka kwa familia za marehemu  na asubuhi ya leo ndipo alipopata  taarifa yakupatikana kwa miili yao katika bwawa hilo.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Rajab Ali Rajab amesema taarifa za tukio hilo zinasema vijana hao wanasadikiwa kuwa huenda ni miongoni mwa watu waliokuwa wanakimbia  Askari wa Jeshi la Polisi lililokuwa linafanya doria katika vijiji vinavyofanya biashara ya ulevi na dawa za kulevya.

Hata hivyo ameitaka jamii kuacha tabia ya kutumia ulevi ili kujiepusha na vitendo kama hivyo ambavyo vinasababisha maafa  pamoja na taifa kupoteza nguvu kazi yake.

Maiti hizo  zimeokolewa kutoka katika bwawa hilo na kikosi cha zimamoyo na tayari zimekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Story na Rauhiya Mussa Shaaban.

Chanzo: Zanzibar 24