0
Menu
Infos

Uvuvi wa kutumia mabomu wapungua

Uvuvi wa kutumia mabomu wapungua

Wed, 18 Nov 2020 Source: HabariLeo

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (anayeshughulikia uvuvi), Dk Rashid Tamatamah amesema uvuvi haramu kwa kutumia mabomu katika bahari nchini umepungua kwa karibia asilimia 100.

Dk Rashid aliyasema hayo mjini Pangani wakati wa ziara yake ya siku moja ya kuangalia ujenzi wa ofisi za vikundi shirikishi vya ulinzi wa rasilimali za uvuvi (BMU) hiyo Kata ya Kipumbwi huku akioneshwa kuridhishwa na kazi ya ujenzi wake.

Ujenzi unatekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya ufadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi unaoitwa Swiofish na ujenzi ni moja vitu ambavyo vimeazimiwa kutekelezwa katika mradi huo wa miaka sita ambao utaisha mwakani.

Alisema katika vitu vya kutekelezwa ni kujenga majengo ya ofisi za BMU tano kwenye ukanda wa Pwani. Walitaka kila mahali wajenge lakini fedha zilizopo zilikuwa hazitoshi, hivyo wakachagua maeneo matano ambayo ni Lindi, Bagamoyo, Saadani, Kipumbwi na Zanzibar.

Alisema serikali katika kipindi chake cha kwanza ilipokuwa inaanza kazi hali ya uvuvi nchini ilikuwa mbaya kutokana na kukithiri kwa uvuvi haramu.

Alieleza kwamba baada ya serikali kuingia mwaka 2017 ikaamuliwa kwamba kama hali hiyo ingeendelea, rasilimali za uvuvi zingetoweka.

"Hivyo serikali ikaamua kuchukua hatua za makusudia kuanzisha operesheni za uvuvi haramu, kwenye maziwa waliita operesheni Sangara na kwenye ukanda wa pwani kulikuwa na operesheni Jodari ambazo ziliwasaidia walikuwa wanawashirikisha BMU,"alisema Katibu Mkuu huyo.

Alisema kwa upande wa Pwani, meli za nje zilikuwa zinapewa leseni za kuvua na ilikuwa ya masharti kwamba wanavua samaki wa aina fulani lakini wakawa wanavua samaki ambao ni nje ya leseni.

"Kuna meli iliyokuwa inatoka Vietnam ilikamatwa ikiwa na mapezi ya papa, ilishikiliwa, serikali ikafungua kesi ikaendeshwa tukashinda ikapigwa faini ya Sh bilioni moja au waende jela, na wameenda jela,"alisema.

Akizungumzia kwenye Ziwa Victoria alisema wamefanikiwa kutokomeza uvuvi haramu kwa zadi ya asilimia 80 lakini bado hawajamaliza kabisa kutokana na matumizi ya nyavu haramu.

Alisema miaka ya nyuma kote Tanzania haijawahi kuwa na samaki ambao wanazalishwa kufikia tani 400,000 ambazo zinazalishwa kwa mwaka lakini baada ya operesheni hizo kwa mwaka 2018/19 kwa mara ya wamefika tani 448,000 huku mwaka uliopita walipata tani 497,000.

Katibu huyo alisema kwa upande wa ziwa Tanganyika viwanda vingi vya minofu inayopelekwa nje ni vya sangara hivyo viwanda huko vilifungwa kutokana na uwepo wa uvuvi haramu.

Alisema zamani nchini kulikuwa na viwanda 12 hadi 13 lakini kutokana na uvuvi haramu vilikufa na kubaki vinane na vingi vilikufa kutokana na kukosa malighafi.

Aidha alisema hakukuwa na samaki wa kupelekwa viwandani ambavyo vilikuwa na uwezo wa kuchakata tani 40 kwa siku lakini vilichakata tani tatu mpaka tano kwa siku kwa hiyo wafanyakazi ajira zilipotea.

"Baada ya kufanikiwa kukomesha uvuvi harama samaki wameongezeka na viwanda vinazalisha muda wote na sasa kuna viwanda vinne vinajengwa,"alisema.

Chanzo: HabariLeo