0
Menu
Infos

Utafiti sekta ya uvuvi nchini waimarishwa

Utafiti sekta ya uvuvi nchini waimarishwa

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia uvuvi, Dk Rashid Tamatamah amesema serikali imetilia mkazo utafiti katika sekta ya uvuvi nchini ili kuwezesha kupatikana taarifa sahihi juu ya maeneo ya uvuvi, uzalishaji vifaranga bora vya samaki, pamoja na chakula bora cha samaki.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa maabara ya kisasa ya utafiti wa uvuvi itakayotumiwa na Taasisi ya Uvuvi Tanzania(Tafiri) inayojengwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (Swiofish).

Dk Tamatamah alisema mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa mkopo wa masharti nafuu wa Sh bilioni 2.6 na unalenga kukuza sekta ya uvuvi nchini.

"Kwenye uchumi wa buluu katika awamu hii tunategemea meli nane kwenye uvuvi wa bahari kuu, unapofanya uvuvi wa bahari kuu haujiendei tu lazima watafiti kama Tafiri waende baharini wajue chambo wanapata wapi kwa ajili ya kuvua samaki.”

“Pia tuna mpango wa kuongeza uzalishaji wa samaki kupitia ufugaji kwenye maeneo mawili ya chakula bora pamoja na vifaranga bora hivyo tafiti ni muhimu kupitia maabara hii," alisema.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo serikali itapunguza au kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa vifaranga bora vya samaki na chakula bora cha samaki kutokana na watu wengi kujitokeza kufuga samaki ambapo mahitaji ni vifaranga milioni 50 kwa mwaka lakini kwa sasa vinavyozalishwa hapa nchini ni milioni 30 pekee.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Swiofish Tanzania Bara, Nichrous Mlalila alisema baada ya kukamilika kwa jengo hilo wataalamu watajikita kufanya tafiti kwani kwa sasa sampuli za mazao ya samaki zimekuwa zikisafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya tafiti hali ambayo inahatarisha usalama wa nchi na rasilimali zake.

Aidha, alisema serikali inatarajia kujenga maabara nyingine kupitia mradi huo kwa ajili ya kuzalisha vifaranga bora vya samaki wa baharini pamoja na mbegu za zao la mwani katika kukuza sekta ya uvuvi hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Tafiri, Dk Ismael Kimirei alisema taasisi hiyo ina mikakati mingi katika kukuza tafiti za uvuvi hapa nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa pamoja na kupunguza gharama za kutuma sampuli za uvuvi kwenda nchi za nje.

Mradi wa Swiofish unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ulianza kazi hapa nchini Juni, 2015 na unatarajia kukamilika Mei, 2021.

Hata hivyo, serikali ina matumaini makubwa ya mradi huo kuendelea kuwapo nchini kutokana na matokeo chanya katika kukuza sekta ya uvuvi ambapo ujenzi wa maabara hiyo unatarajia kuwa umekamilika na kukabidhiwa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Desemba 8, mwaka huu.

Chanzo: HabariLeo