0
Menu
Infos

Ushauri wa TMA uzingatiwe kikamilifu kuepuka madhara

Ushauri wa TMA uzingatiwe

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

MVUA za msimu zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwa ni mwanzo wa msimu wa vuli na zinatarajiwa kuendelea kunyesha hadi Desemba 2020 tangu zilipoanza mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.

Kulingana na utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), katika maeneo mengi ya nchi ambayo yanapata misimu miwili mvua hizo zitakuwa wastani na chini ya wastani ikiwa ni ishara kuwa msimu huu kutakuwa na upungufu wa mvua ikilinganishwa na msimu uliopita.

Maeneo hayo ambayo ni pamoja na Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba, Kusini mwa Mkoa wa Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Ni kutokana na hali hiyo ndiyo maana TMA ikatoa ushauri kuwa kutokana na hali hiyo wakulima na wafugaji wachukue hatua stahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na upungufu wa mvua hizo.

Kwa mujibu wa TMA kutakuwa na upungufu wa unyevunyevu katika udongo katika maeneo mengi ya nchi hali ambayo haitakuwa nzuri kwa wakulima na wafugaji. Kutokana na utabiri huo wakulima walishauriwa kuwa makini kutokana na mazao wanayopata yaendane na hali hiyo.

Wafugaji wanatakiwa kuwa makini na kujiandaa kutokana na utabiri huu kwa sababu kutakuwa na upungufu wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo yao hivyo wajipange kukabiliana na hali hiyo.

Pia wafugaji na wakulima wajizuie kuchoma moto hovyo kwa sababu kutokana na uhaba wa mvua katika kipindi hicho kwa sababu kutakuwa na hatari ya kutokea kwa majanga ya moto katika misitu na mapori kutokana na ukavu unaotarajiwa.

Kwa upande wa mvua za masika mwelekeo wa mvua hizo za msimu katika maeneo yanayopata mvua msimu mmoja kwa mwaka kuanzia Novemba hadi Aprili 2021 hali inaonesha kuwa ya kuridhisha kidogo kutokana na kuwepo kwa unyevunyevu wa kutosha katika udongo hali itakayoleta afadhali katika sekta ya kilimo na ufugaji.

Katika kipindi hiki TMA imetabiri kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani hivyo ni fursa kwa wakulima kujiandaa vyema kuzitumia kwa ajili ya uzalishaji. Wakulima wanatakiwa kujua kuwa mazao yanayotakiwa katika kipindi hiki cha msimu wa vuli yawe yenye kuvumilia hali ya ukavu.

Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua hizo ni pamoja na Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, Kigoma, Rukwa, Kusini mwa Mkoa wa Morogoro na Mashariki mwa Mikoa ya Katavi na Tabora.

Wananchi katika maeneo hayo wanatakiwa kuwa makini kwa kuwa kutakuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo machache hivyo kutakuwa na hatari ya kutokea mafuriko, mikusanyiko mikubwa ya maji hali inayoweza kusababisha uchafunzi wa maji safi hali inayoweza kuchochea magonjwa ya mlipuko.

Nawakumbusha wananchi kufuata kikamilifu ushauri unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kuwa salama wao pamoja na mali zao. Ikiwa watafuata ushauri huo kikamilifu uwezekano wa kutokea njaa hapa nchini ni mdogo sana kwa kuwa watakuwa na uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha.

Chanzo: HabariLeo