0
Menu
Infos

Tathmini ya NEC yaonesha uchaguzi ulifuata utaratibu

1e564075aeec93e3cc994c9c2f464701 Tathmini ya NEC yaonesha uchaguzi ulifuata utaratibu

Sat, 21 Nov 2020 Source: HabariLeo

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefanya tathimini ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kusema ulifanyika kwa kufuata utaratibu , kushirikisha wadau mbalimbali wakiwamo watazamaji wa ndani na nje wapatao 5,400 waliokwenda hadi vijijini bila kuzuiliwa na kuandika ripoti zao.

Imeeleza ilivyozingatia sheria na taratibu katika masuala mbalimbali ikiwamo kuamua rufaa ikisema, asilimia 17 ya wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani ambao walishindwa kurudishwa baada ya kukata rufaa, ilitokana na kukosa sifa na kwamba hata wakienda mahakamani kufungua kesi, hawawezi kushinda.

Mkurugenzi wa NEC, Dk Wilison Mahera alisema wakati uchaguzi ulifanyika kwa kutumia fedha za ndani, yapo mashirika yaliyokuwa tayari kusaidia uchaguzi lakini kwa kuweka masharti jambo ambalo serikali haikukubali bali ilihitaji kuwa huru.

Akizungumza jana wakati wa kikao kikao cha tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kilichoshirikisha wakurugenzi wa uchaguzi, Mahera alisema uchaguzi ulifuata taratibu zote ikiwamo kuteua wagombea, kushirikisha asasi 245 zilizopewa vibali vya kutoa elimu huku waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje wapatao 5,400 kutoka asasi 97 za ndani na 17 za kimataifa.

" Ushirikishwaji wa wadau ulikuwa mkubwa, ingawa kuna baadhi ya asasi ambazo tulizipa kibali cha cha kutoa elimu ya uchaguzi hazikufanya kutokana na wao kukosa fedha, lakini kwa upande wa waagalizi wa uchaguzi wote walifanya kazi zao bila kuzuiliwa na walikwenda hadi vijijini na wameandika ripoti zao," alisema.

Hata hivyo, Dk Mahera alisema Tume imekuwa ikipokea malalamiko na simu nyingi kutoka kwa baadhi ya wagombea wa ubunge viti maalumu wakidai kuwa imewakata majina jambo alilotaka, wawasiliane na vyama vyao.

" Wanaotupigia simu na kutusumbua wakiamini sisi ndio tunaokata majina waache maana jukumu hilo si letu hivyo wawasiliane na vyama vyao kujua ni kwa nini hawamo kwenye orodha, sisi tunaletewa majina mengi yakiwa na vipaumbele vya chama."

Alisema kutokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata asilimia 78 ya kura zote halali za wabunge na Chadema kupata asilimia 15, Tume imeshapeleka bungeni majina 94 huku Chadema wakiwa kwenye mchakato wa kupeleka majina hayo.

Akizungumzia rufaa, “Rufaa zilizoletwa Tume zilikuwa za wagombea kwa wagombea, na waliokosa ni kwamba hawakuwa na sifa kabisa na hata wakienda mahakamani hawezi kushinda." Kuhusu rufaa, Dk Maherea alisema asilimia 83 ya rufaa zilizokatwa waliwarejesha kwenye uchaguzi huku asilimia 17 ikikosa fursa hiyo.

Aidha, Dk Mahera alisema wiki ijayo Tume itatangaza viti maalumu vya madiwani baada ya jana kupitia majina yaliyowasilishwa na vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa Mahera, katika nafasi ya madiwani, CCM imeshinda viti 3,792, Chadema 87, ACT- Wazalendo 41, CUF viti 18, DP kiti kimoja na NCCR-Mageuzi viti vitatu.

Tathimini ya NEC inaonesha pia kumekuwapo ongezeko la vyama vilivyoshiriki uchaguzi kwa nafasi ya urais hadi kufikia vyama 15 ikilinganishwa na vyama vinane mwaka 2015.

Pia ushiriki wa wanawake uliongezeka kutoka na kuwapo wagombea wawili walioshiriki nafasi ya rais na watano makamu ya rais wakati uchaguzi wa mwaka 2015 walikuwa wawili pekee.

Kwa upande wa utangazaji matokeo, ilifanikiwa kufanya hivyo ndani ya saa 48 ikiwa ni tofauti na saa 72 zilizotumika kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

Kuhusu changamoto, Dk Mahera alitaja kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa kutotii wito wa kamati ya maadili na ukiukwaji wa maadili wakati wa mchakato mzima wa kampeni.

Nyingine ni kuwapo idadi kubwa ya rufaa ikilinganishwa na mwaka 2015 na kwamba tume itaifanyia kazi uchaguzi ujao tatizo lisijirudie au iwe kwa kiasi kidogo.

Changamoto nyingine ilikuwa ni vitisho na lugha za matusi vilivyokuwa vikitolewa na baadhi ya viongozi wa vyama kwa wasimamizi na wakurugenzi wa uchaguzi kwa njia ya simu.

Awali, akifungua kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa Mbarouck Mbarouck alisema shughuli ya tathimini hufanyika baada ya uchaguzi ikiwa na madhumuni ya kupata mrejesho wa namna gani uchaguzi umeendeshwa.

Chanzo: HabariLeo