0
Menu
Infos

Tangi la maji Ilemela kukamilika mwakani

91e891b0bf65f6e836d74e334e9b3d68.jpeg Tangi la maji Ilemela kukamilika mwakani

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

MRADI wa ujenzi wa tanki la maji katika kata Buswelu, wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza lenye ujazo wa lita milioni tatu unatarajiwa kukamilika Juni mwakani.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo juzi, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Leonard Msenyele alisema ujenzi huo ukikamilika utatatua kero ya maji katika wilaya ya Ilemela na maeneo mbalimbali mkoani hapa.

Alisema mradi huo upo chini ya mtaalamu mshauri Egis na ICE Tanzania, huku mkandarasi mkuu ni kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).

Msenyele alisema mpaka mradi huo kukamilika utagharimu Sh bilioni 5.1 na wahisani wa mradi ni Serikali ya Tanzania, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFB).

Alisema kazi zinazoendelea katika mradi huo kwa sasa ni kuandaa umwagaji wa zege ya awali, kuandaa kitako cha tanki, kukusanya mchanga na kokoto pamoja na kuchimba mawe.

Msenyele aliyataja maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni Buswelu, Lukobe, Kigala, Nsumba na Kahama.

Alisema kazi zingine zinazoendelea ni kutengeneza barabara ya kuelekea kwenye tanki na umwagaji wa zege kuta za tangi.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk Mathias Lalika aliishukuru serikali kwa kuweka mradi huo mkubwa wa maji wilayani kwake.

Chanzo: HabariLeo